Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema mikopo inayochukua Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hukuza mitaji ya mashirika ya umma na kuzalisha faida kwa nchi na wananchi.
Ametolea mfano mkopo uliojenga miradi kama ya Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP), inapokamilika, fedha hizo hugeuka kuwa mtaji wa kuwezesha mashirika ya umma.
Mchechu ameyasema hayo leo, Jumanne Juni 30, 2026 alipozungumza katika Siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Amesema wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani mtaji wa taasisi zote ya umma ulikuwa Sh67 trilioni, lakini sasa umefikia Sh92 trilioni. Sawa na ongezeko la asilimia 37.
Kiasi hicho cha ukuaji wa zaidi ya asilimia 20, amesema ni mchanganyiko wa vitu vingi, ikiwemo mikopo ambayo Serikali inachukua kuwekeza kwenye mashirika na uzalishaji na kukua kwa mitaji.
“Hata huku tulipo tunapojenga Reli ya Kisasa (SGR) sasa hivi ni mkopo, lakini ile fedha SGR itakapokamilika ile fedha yote itatumika kama mtaji ndani ya Shirika la Reli (TRC),” amesema.
Ameeleza vivyo hivyo hata kwa fedha za mkopo wa ujenzi wa mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JHPP) na miradi yote itakapokamilika mtaji utafikia Sh130 trilioni.




