HomeAfyaFloton Africa yatoa milioni 30/- kusaidia uanzishwaji wa kituo cha matibabu maalumu

Floton Africa yatoa milioni 30/- kusaidia uanzishwaji wa kituo cha matibabu maalumu

UNGUJA:  Kampuni ya Floton Africa imetoa msaada wa Sh30 milioni kwa ajili ya kusaidia uanzishwaji wa Kituo Maalumu cha Upandikizaji wa Uboho na Matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya uchangishaji fedha inayolenga kupanua upatikanaji wa huduma za matibabu bingwa nchini Tanzania.

Msaada huo ulikabidhiwa Jumatano na Mkurugenzi wa Floton Africa, Swapna Brahmaroutu, kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali na wadau mbalimbali.

Fedha hizo zitasaidia juhudi za kuanzisha huduma maalumu za matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za upandikizaji wa uboho, huku pia zikichangia juhudi za kitaifa za kuboresha huduma kwa wagonjwa wa selimundu pamoja na wanaohitaji kupandikizwa figo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Bi Brahmaroutu alisema mchango huo unaonesha dhamira ya kampuni ya kuwekeza kwa watu sambamba na maendeleo ya miundombinu.

“Katika Floton Africa tunaamini kuwa maendeleo endelevu hayaishii kwenye ujenzi wa majengo na miundombinu pekee. Yanahusisha pia kuwekeza kwa watu, kuimarisha huduma za afya na kujenga jamii zenye afya bora. Tunajivunia kuunga mkono mpango huu muhimu na tuna matumaini kuwa mchango wetu utaleta matumaini na kuboresha huduma za afya kwa familia nyingi,” alisema.

Kampeni hiyo ya uchangishaji fedha ilizinduliwa wakati Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na lengo la kupanua huduma za matibabu bingwa ambazo awali hazikupatikana nchini.

Baada ya kupokea mchango huo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, alisema kampeni hiyo inaratibiwa kitaifa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), huku Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakihamasisha wananchi na wadau katika maeneo yao kuchangia.

Alisema huduma za matibabu bingwa zinazotolewa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa sasa zinawanufaisha wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo kupunguza ulazima wa wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

“Tunawahamasisha watu binafsi, kampuni na wawekezaji kuchangia katika jambo hili muhimu. Tunawashukuru Floton Africa kwa kuungana nasi kwa kutoa Sh30 milioni na tunatoa wito kwa wawekezaji wengine katika mkoa wetu kujitokeza kuunga mkono kampeni hii,” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kampeni ya uchangishaji itaendelea hadi Julai 11, ambapo kutafanyika hafla ya kitaifa ya kuchangisha fedha jijini Dodoma.

Floton Africa, yenye uwekezaji katika eneo la Paje, Zanzibar, ilisema mchango huo ni sehemu ya mpango wake mpana wa uwajibikaji kwa jamii unaojikita katika sekta za afya, elimu, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii.

Kampuni hiyo ilieleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kutekeleza miradi yenye manufaa ya kudumu kwa jamii na inayochangia maendeleo endelevu ya Tanzania.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments