Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini imeendelea kuandika historia katika sekta ya afya nchini baada ya kuwa hospitali ya kwanza Tanzania kuwapatia huduma ya upandikizaji wa uume wanaume 14 na kupata mafanikio kutokana na kufanya kazi vizuri.
Hayo yameelezwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa BMH, Dk. Abdallah Baja wakati akitoa taarifa kuhusu mafanikio hayo na mengine ikiwa ni kuelekea Maadhimisho ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo.
Dk. Baja, anasema wanaume hao wamefanyiwa upandikizaji wa uume tangu hospitali hiyo kuanza kutoa huduma hiyo mwaka 2023 huku wakiendelea vizuri.
Anasema licha ya kuwepo kwa huduma hiyo, bado wanaume wengi wenye changamoto hiyo, wamekuwa wakisita kujitokeza kutokana na aibu au hofu ya kueleza matatizo yao kwa wataalamu wa afya.
Dk. Baja anasema matibabu hayo yana uwezo wa kumrejeshea mgonjwa hali ya kawaida baada ya kufanyiwa upandikizaji, kurejesha afya na kuimarisha maisha ya familia na kijamii.
Anasisitiza kuwa hospitali hiyo inawahimiza wanaume wenye changamoto ya kutofanya kazi kwa ufanisi kwa uume kujitokeza kupata ushauri na matibabu stahiki badala ya kuendelea kuteseka kimya kimya.




