Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unashiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, ukiwahakikishia wanachama na wananchi huduma mbalimbali pamoja na elimu kuhusu hifadhi ya jamii.
Akizungumza katika banda la PSSSF, Afisa Mkuu wa Uhusiano wa Mfuko huo, Bi. Rehema Mkamba, amesema maonesho ya Sabasaba ni fursa muhimu ya kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, kuwahudumia, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi papo kwa papo, pamoja na kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali kupitia PSSSF Portal inayopatikana kwenye simu za mkononi.


Amesema kupitia huduma hizo za kidijitali, wanachama na wastaafu wanaweza kupata taarifa za michango yao, kufuatilia mafao, kuwasilisha madai, kuhuisha taarifa za wategemezi, kuuliza maswali mbalimbali na kwa upande wa wastaafu kujihakiki kwa urahisi.
Bi. Mkamba amesema kaulimbiu ya PSSSF katika maonesho hayo inaendana na kaulimbiu ya Sabasaba ya mwaka huu inayosema, “Sabasaba, Fahari ya Tanzania,” huku Mfuko ukisisitiza dhamira yake ya “Kumhakikishia mwanachama kesho ya uhakika kwa kuwahudumia wanachama.”
Aidha, amesema wananchi watakaotembelea banda la PSSSF watapata pia fursa ya kujionea uwekezaji mbalimbali unaofanywa na Mfuko huo katika viwanda pamoja na majengo ya biashara na makazi.
“Njoo uone na ufaidike na uwekezaji wa PSSSF kwa kujipatia nyama bora yenye viwango vya kimataifa, pamoja na bidhaa za ngozi zikiwemo viatu, mikoba na mikanda,” amesema Bi. Mkamba, huku akiwakaribisha wanachama na wananchi wote kutembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Sabasaba.





