HomeHabari‎MD Twange  afafanua chanzo hitilafu iliyotokea Gridi ya Taifa

‎MD Twange  afafanua chanzo hitilafu iliyotokea Gridi ya Taifa

📌‎ Aomba radhi kwa wateja wananchi na kuwahakikishia upatikanaji endelevu wa huduma ya umeme

‎📌 Asema uzalishaji wa umeme umefikia megawati 4400 na juhudi za kuimarisha Mfumo wa Gridi zinaendelea

‎Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amewaomba radhi wananchi na wateja wote wa huduma ya umeme kufuatia hitilafu iliyotokea kwenye Mfumo wa Gridi ya Taifa Juni 27, 2026, na kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

‎Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 28, 2026, Twange amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa hitilafu hiyo ilisababishwa na matatizo yaliyojitokeza kwa wakati mmoja katika njia tatu za usafirishaji wa umeme pamoja na mashine moja ya kuzalisha umeme.

‎Amefafanua kuwa Gridi ya Taifa ni mfumo mmoja unaounganisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, hivyo hitilafu kubwa katika sehemu yoyote ya mfumo huo inaweza kuathiri gridi nzima na kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo mengi kwa wakati mmoja.

‎”Tunatambua usumbufu uliowakumba wananchi na wateja wetu kutokana na hitilafu hii, na tunawaomba radhi. Wataalamu wetu walifanya kazi usiku kucha kuhakikisha huduma ya umeme inarejea kwa haraka na kwa usalama,” amesema Twange.

‎Amesema huduma ya umeme ilirejeshwa usiku huohuo na kwa sasa mikoa yote pamoja na Zanzibar inaendelea kupata umeme kama kawaida.

‎Twange ameeleza kuwa kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani megawati 4,400 za umeme kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo gesi asilia, maji na nishati ya jua, kiwango kinachotosheleza mahitaji ya sasa ya nchi.

‎Amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya umeme, huku TANESCO ikiwa na mtandao wa zaidi ya kilomita 8,000 za njia kuu za kusafirisha umeme pamoja na vituo mbalimbali vya kupokea na kusambaza umeme vinavyounda Mfumo wa Gridi ya Taifa.

‎Kwa mujibu wa Twange, hitilafu ya jana ilikuwa ya kipekee kutokana na kutokea kwa matatizo katika maeneo kadhaa kwa wakati mmoja, hali iliyosababisha mfumo mzima wa gridi kuathirika.

‎Amesema TANESCO ina mifumo ya kisasa ya kiteknolojia inayofuatilia hali ya gridi muda wote na ndiyo iliyowezesha kubaini mara moja maeneo yaliyopata hitilafu.

‎”Tunatumia teknolojia za kisasa zinazotuwezesha kupata taarifa za hitilafu mara moja. Mfumo wetu ulitoa taarifa kuwa kulikuwa na matatizo katika njia tatu za usafirishaji wa umeme pamoja na mashine moja ya kuzalisha umeme, jambo lililowawezesha wataalamu wetu kuchukua hatua kwa haraka,” amesema.

‎Aidha, amesema shirika linaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo akili mnemba (AI) ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

‎Amebainisha kuwa ndani ya wiki ijayo TANESCO itazindua mfumo wa Chatbot, utakaowezesha wateja kupata majibu ya maswali yao moja kwa moja kupitia mfumo wa kidijitali bila kulazimika kuwasiliana na wahudumu.

‎Twange amesema TANESCO inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha uthabiti wa Gridi ya Taifa kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kupunguza uwezekano wa kujirudia kwa hitilafu kama hiyo.

‎Amesisitiza kuwa lengo la shirika ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya umeme ya uhakika, salama na endelevu huku likiendelea kutoa taarifa sahihi kwa wakati kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme.

‎Pia amewashukuru waandishi wa habari kwa kusaidia kufikisha taarifa kwa wananchi wakati wa hitilafu hiyo, akisema ushirikiano huo umechangia kuwafahamisha wateja hatua zilizokuwa zikichukuliwa kurejesha huduma

‎Twange amewahakikishia wananchi kuwa TANESCO itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya umeme ili kuhakikisha huduma inakuwa ya uhakika na inakidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi na jamii.


RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments