HomeMichezoCRDB Bank Bunge Grand Bonanza kipenga kimepulizwa

CRDB Bank Bunge Grand Bonanza kipenga kimepulizwa

DAR ES SALAAM: Benki ya CRDB leo imekabidhi vifaa vya michezo pamoja na zawadi zitakazotolewa kwa washindi wa CRDB Bank Bunge Grand Bonanza litakalofanyika  tarehe 20 Juni 2026 katika Uwanja Jamhuri mkoani Dodoma ambako mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa amesema wametenga jumla ya shilingi milioni 450 kufanikisha bonanza hilo ambalo mwaka huu litawahusisha pia mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

TullyEsther amesema uhusiano imara uliopo kati ya Benki ya CRDB na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unawahusisha pia waheshimiwa wabunge ambao ni wateja muhimu wa benki.

“Ushirikiano wetu hauishii kwenye huduma za fedha pekee bali unaimarishwa zaidi kupitia shughuli za kijamii na maendeleo ya wananchi, ikiwamo utekelezaji wa Programu ya Imbeju inayosimamiwa na taasisi ya CRDB Bank Foundation yenye kusudi la kukuza elimu ya fedha, kujenga uchumi jumuishi na uwezeshaji wa mitaji kwa wananchi,” amesema TullyEsther.

Mkurugenzi amemkabidhi Mwenyekiti Bunge Bonanza, Festo Sanga trakisuti 1,000, fulana 1,000, jezi za mpira wa miguu seti mbili, jezi za mpira wa pete seti mbili, jezi za mpira wa kikapu seti nne na jezi za mpira wa wavu seti nne. Vifaa vingine ni kofia 1,000, medali 1,200 pamoja na makombe tisa.

Akipokea vifaa hivyo, Sanga amesema bonanza hili litaanza kwa matembezi kisha kuendelea kwa michezo ya bao na karata kabla jioni timu za wabunge hazijapambana na mabalozi katika mpira wa miguu, huku kwenye mpira wa pete na mpira wa kikapu wakikutana na wafanyakazi wa Benki ya CRDB.

“Mchezo ni mashabiki hivyo tunawaalika Watanzania wote kujitokeza na kuwashabikia wabunge na viongozi wao huku wakijifunza umuhimu wa afya kupitia michezo,” amesisitiza Sanga.

Sanga ameipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha bonanza hilo na kukuza michezo nchini.

“Ushirikiano huu na Benki ya CRDB ni kielelezo cha namna sekta binafsi na taasisi za umma zinavyoweza kushirikiana kuhamasisha michezo, kujenga afya njema na kuimarisha umoja miongoni mwa viongozi na wananchi kwa ujumla,” amesema.

Akiwa ameshiriki mbio za CRDB Bank Marathon nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mheshimiwa Sanga amesema: “Ukienda kwenye haya mataifa na ukaona jinsi mbio hizi zinavyofanyika utaiona nguvu ya diplomasia ya michezo ambayo inawaunganisha watu wengi bila kujali hali zao za kiuchumi. Mwaka huu katika CRDB Bank Bunge Grand Bonanza tumewakaribisha mabalozi ili kutanua wigo wa ushirikiano wetu na kuimarisha diplomasia ya michezo kati ya Tanzania na mataifa mengine tunayohusiana.”

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments