HomeHabariMasauni: Miradi sita ya kaboni yafikia hatua ya uzalishaji

Masauni: Miradi sita ya kaboni yafikia hatua ya uzalishaji

Tanzania imepiga hatua katika kuendeleza soko la kaboni, huku miradi sita ikifikia hatua ya kuzalisha krediti za kaboni, hatua inayotarajiwa kufungua fursa za uwekezaji wa kijani, uhifadhi wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema hayo Oktoba 14, 2026, jijini Kigali, Rwanda, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026, unaowakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji, wanunuzi wa krediti za kaboni, waendelezaji wa miradi na taasisi za kifedha za maendeleo.

Masauni amesema hatua hiyo inaonesha maendeleo ya Tanzania katika kujenga soko la kaboni lenye mifumo madhubuti ya usimamizi, uwazi na uadilifu, huku likilenga kuchangia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kukuza maendeleo endelevu.

Ameeleza kuwa katika kikao cha mwisho cha Kamati ya Taifa ya kutathmini miradi ya kaboni, miradi minne iliyofikia hatua ya ukomavu iliidhinishwa. Miradi hiyo inahusisha nishati safi ya kupikia pamoja na manufaa ya kijamii, na hatua hiyo imeisogeza mbele katika mchakato wa kuzalisha krediti za kaboni zinazoweza kuthibitishwa.

“Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisera na kitaasisi inayosimamia shughuli za biashara ya kaboni ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inatoa matokeo chanya katika uhifadhi wa mazingira na kuleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi,” amesema Masauni.

Ameongeza kuwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2025, Serikali imeanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), chenye jukumu la kusajili miradi, kusimamia upimaji na uhakiki wa matokeo pamoja na kuzuia kuhesabiwa mara mbili kwa matokeo ya miradi ya biashara ya kaboni.

Akizungumzia fursa za soko la kaboni barani Afrika, Masauni amezitaka nchi za Afrika kutumia mkutano huo kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji, wanunuzi, waendelezaji wa miradi na taasisi za kifedha za maendeleo ili kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa mazingira.

Amesema ni muhimu kuunganisha miradi inayokidhi viwango vya ubora na mahitaji halisi ya soko, kuhakikisha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kuimarisha mifumo ya upimaji na uthibitishaji wa matokeo na kuhakikisha wananchi wananufaika na mapato pamoja na fursa zinazotokana na miradi hiyo.

Masauni amesisitiza pia umuhimu wa nchi za Afrika kujenga uwezo wa kitaalamu na kiuongozi katika sekta ya kaboni ili ziweze kushiriki kikamilifu katika soko la kimataifa na kuchangia maamuzi kuhusu mwelekeo, kanuni na viwango vya soko hilo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Kathryn Kigaraba, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya kaboni kujadili namna ya kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza utekelezaji wa miradi na kujenga soko lenye uaminifu na manufaa kwa jamii.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Immaculate Semesi, amesema baraza hilo litaendelea kushirikiana na NCMC kusimamia na kufanikisha miradi ya kaboni ili kulinda mazingira na kuhakikisha wananchi wananufaika.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments