HomeBiasharaTVLA yaelimisha wauzaji wa pembejeo kuhusu matumizi ya chanjo

TVLA yaelimisha wauzaji wa pembejeo kuhusu matumizi ya chanjo

Wauzaji wa pembejeo za mifugo katika mikoa ya Rukwa na Songwe wamepatiwa elimu kuhusu utambuzi, uhifadhi na matumizi sahihi ya chanjo, hatua inayolenga kusaidia wafugaji kupata bidhaa zenye ubora na kupunguza hatari ya magonjwa ya mifugo.

Elimu hiyo imetolewa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kupitia ziara iliyofanyika Oktoba 19 hadi 22, 2026, iliyoongozwa na Meneja wa Kituo cha Kanda ya Kusini Magharibi, Dk. Rajabu Mlekwa, kwa kushirikiana na wataalamu wa masoko kutoka makao makuu ya wakala huo.

Timu hiyo imetembelea wauzaji wa pembejeo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.

Katika ziara hiyo, wauzaji wameelezwa huduma mbalimbali zinazotolewa na TVLA, zikiwamo uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uzalishaji na usambazaji wa chanjo, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, pamoja na usajili na udhibiti wa ubora wa viuatilifu vya mifugo.

Huduma nyingine ni utafiti wa magonjwa ya wanyama na wadudu wanaoeneza magonjwa hayo, pamoja na utoaji wa ushauri na mafunzo kwa wadau wa sekta ya mifugo.

Kwa upande wa chanjo, wauzaji wamepatiwa maelekezo kuhusu namna ya kutambua chanjo zinazozalishwa na TVLA, kuzihifadhi katika mazingira yanayofaa na kufuata maelekezo ya matumizi ili kudumisha ubora na ufanisi wake.

TVLA imelenga kuwajengea uwezo wauzaji hao kwa kutambua nafasi yao katika kuwafikia wafugaji na kuwapa taarifa sahihi kuhusu matumizi ya chanjo na huduma nyingine za afya ya mifugo.

Uelewa huo pia unatarajiwa kuwasaidia wauzaji kuwaelekeza wafugaji kwenye huduma za uchunguzi wa magonjwa maabara, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo na ushauri wa kitaalamu kuhusu changamoto za afya na uzalishaji.

Kupitia ziara hiyo, TVLA inaendelea kuimarisha ushirikiano na wauzaji wa pembejeo na kusogeza elimu kuhusu huduma zake karibu na wadau, kwa lengo la kulinda afya ya mifugo na kuongeza tija katika ufugaji nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments