Tanzania inalenga kutumia soko la kaboni kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na mapato ya jamii, pamoja na kuhifadhi mazingira, huku Serikali ikiimarisha mifumo ya usimamizi na uwazi ili kuhakikisha biashara hiyo inaleta manufaa kwa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema hayo Oktoba 22, 2026, wakati akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026 lililofanyika Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu isemayo “Siku Moja. Soko Moja. Maono ya Pamoja.”
Masauni amesema Serikali inalenga kuifanya biashara ya kaboni kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kwa kuchochea uwekezaji, kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya jamii, kuhifadhi misitu na kuendeleza matumizi ya nishati safi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tanzania imeamua kuwa kitovu cha soko la kaboni lenye uadilifu barani Afrika, soko ambalo kila tani ya kaboni inayothibitishwa inatafsirika kuwa ajira kwa vijana wetu, mapato kwa vijiji vyetu, misitu iliyohifadhiwa, nishati safi majumbani mwetu na mtaji wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.




Amesisitiza kuwa mafanikio ya soko hilo hayatapimwa kwa idadi ya miradi pekee, bali pia ubora wa matokeo, uzingatiaji wa sheria, uwekezaji unaotekelezwa na manufaa halisi yanayowafikia wananchi.
Ameongeza kuwa ajenda ya nishati safi ya kupikia ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa katika biashara ya kaboni, kutokana na uwezo wake wa kuwafikia mamilioni ya kaya na kuchangia kupunguza uzalishaji wa gesi joto.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Kathryn Kigaraba, amesema kituo hicho kina jukumu la kusaidia maendeleo ya soko la kaboni nchini kwa kutumia utaalamu wa kisayansi, mbinu sahihi za kitaalamu, uwazi wa taarifa na mifumo ya ufuatiliaji na uthibitishaji wa miradi.
Amesema lengo ni kuhakikisha miradi ya kaboni inatambuliwa na kuendelezwa kwa utaratibu unaofaa, inatekelezwa kwa uwazi na manufaa yake yanachangia maendeleo endelevu ya Tanzania.




Kigaraba amesisitiza kuwa kufanikisha azma hiyo kunahitaji ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, waendelezaji wa miradi ya kaboni, wawekezaji, taasisi za fedha, jamii za wenyeji, taasisi za utafiti na washirika wa maendeleo.
Ameongeza kuwa mifumo ya kitaasisi inayohusu tathmini na usajili wa miradi, ubadilishanaji wa taarifa na ulinzi wa haki na maslahi ya wadau ni muhimu katika kujenga imani katika soko hilo.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Richard Muyungi, amesema jamii zinazoshiriki katika usimamizi wa misitu, ardhioevu, mikoko na maeneo mengine yenye uwezo wa kuhifadhi kaboni zinapaswa kuhusishwa kikamilifu katika kubuni na kutekeleza miradi hiyo.
Amesema jamii hizo zinapaswa pia kushiriki katika kupanga namna ya kugawana manufaa yatakayopatikana, huku wanawake, vijana, wajasiriamali wa ndani na waendelezaji wa miradi midogo wakipewa nafasi katika uchumi unaochochewa na soko la kaboni.





