Wednesday, March 4, 2026
spot_img
HomeAfyaNHIF, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kushirikiana kulinda taarifa za wanachama

NHIF, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kushirikiana kulinda taarifa za wanachama

Menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imepokea ujumbe wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Commission – PDPC) ulioongozwa na Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Emmanuel Mkiria, leo jijini Dodoma.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kujenga uhusiano wa kimkakati kati ya taasisi hizo mbili, hasa katika kuhakikisha ulinzi wa taarifa binafsi za wanachama wa NHIF, sambamba na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mkiria alisema PDPC imeanzishwa kwa mujibu wa sheria na kuanza kazi rasmi mwaka 2022, ikilenga kusimamia na kulinda faragha ya wananchi katika zama za ukuaji mkubwa wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Alieleza kuwa NHIF ni miongoni mwa wadau muhimu wa kimkakati wanaohusiana moja kwa moja na ukusanyaji na utunzaji wa taarifa binafsi, hivyo ni muhimu kuweka mifumo imara ya ulinzi wa taarifa hizo.

Katika kikao hicho, pande hizo mbili ziliunda Kamati ya Pamoja ambayo itashughulikia masuala ya kimkakati yakiwemo kujengea uwezo, elimu kwa umma, usimamizi wa ridhaa (Consent Management System) na tathmini ya athari za ulinzi wa taarifa (Data Protection Impact Assessment).

Dkt. Mkiria alishukuru uongozi wa NHIF kwa ushirikiano na kwa kutoa muda wa kujadiliana masuala hayo muhimu ya ulinzi wa taarifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene C. Isaka, alimpongeza Mtendaji Mkuu wa PDPC na ujumbe wake kwa ujio wao, akisisitiza kwamba NHIF imejipanga kikamilifu kulinda taarifa binafsi za wanachama wake.

Alibainisha kuwa watumishi wote wa NHIF wamefanyiwa upekuzi (vetting) na mamlaka husika na wamekula viapo vya kutunza siri, huku madaktari wa Mfuko nao wakifuata taratibu na viapo vya mabaraza yao ya kitaaluma.

Dkt. Isaka alihitimisha kwa kusisitiza kuwa NHIF inatambua umuhimu wa kulinda taarifa za wanachama wake, kwani taarifa hizo ni “bidhaa inayotafutwa” na zinahitaji ulinzi wa hali ya juu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments