HomeHabariRais wa Singapore akoshwa na fursa za uwekezaji Tanzania

Rais wa Singapore akoshwa na fursa za uwekezaji Tanzania

Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore unapaswa kupewa sura mpya inayolingana na mahitaji ya dunia ya sasa, akieleza kuwa lengo la ushirikiano huo ni kuhuisha historia ya mahusiano ya nchi hizo mbili na kuipa umuhimu unaoendana na wakati uliopo.

Rais Shanmugaratnam ameyasema hayo leo, Jumanne Juni 9, 2026 alipozungumza katika Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Singapore, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu nchini.

Amesema dunia imeingia katika kipindi ambacho mifumo na sheria za biashara za kimataifa zimebadilika kwa kiwango kikubwa, huku baadhi ya mabadiliko hayo yakionekana kuwa ya kudumu.

Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa kujenga ushoroba mpya wa fursa za biashara na kuimarisha minyororo ya thamani inayostahimili misukosuko ya kiuchumi.

“Tanzania ni nchi yenye fursa na uwezo mkubwa sana wa maendeleo, na idadi kubwa ya waliojitokeza leo inaonyesha kuwepo kwa hamasa ya kweli na inayoongezeka kuhusu Tanzania pamoja na uhusiano wa Tanzania na Singapore na bara la Asia,” amesema.

Rais huyo amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na kizazi kipya cha wajasiriamali kwa kupanua uwekezaji katika sekta mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa kuunganisha miradi ya maendeleo na masoko ya kimataifa ili kuongeza tija na ushindani.

Ametaja sekta za kilimo biashara, miundombinu, huduma na teknolojia za kidigitali kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa.

Amesema ushirikiano wa Tanzania na Singapore unaweza kuchochea ajira, ustawi wa wananchi na ukuaji jumuishi wa uchumi iwapo pande zote zitakumbatia dira ya pamoja ya maendeleo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments