Benki ya NMB imetangaza kuingia katika awamu mpya ya ukuaji baada ya kukamilisha mpango wake wa muda wa kati wa mwaka 2021 hadi 2025, uliowezesha taasisi hiyo kufikia rekodi ya faida kabla ya kodi ya zaidi ya Sh.trilioni moja.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wawekezaji uliofanyika kuelekea mkutano mkuu wa 26 wa wanahisa wa benki hiyo unaotarajiwa kufanyika leo.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, Ofisa Mkuu wa Fedha, Juma Kimori, pamoja na Mkurugenzi wa Uhusiano na Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano, Innocent Yonazi, waliwasilisha mafanikio ya utekelezaji wa mkakati huo wa miaka mitano na mwelekeo wa benki kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa mujibu wa uongozi wa benki hiyo, kipindi cha miaka mitano kilichomalizika mwaka 2025 kiliimarisha misingi ya ukuaji wa NMB kupitia ongezeko la faida, mali, amana za wateja, mikopo, wateja wapya, huduma za kidijitali na ushiriki mkubwa katika sekta mbalimbali za uzalishaji.


“Hii imekuwa sura muhimu katika historia ya NMB. Mageuzi tuliyoyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano yamejenga taasisi imara zaidi, mtindo wa biashara wenye ustahimilivu na msingi thabiti wa kuingia katika awamu mpya ya ukuaji,” amesema Zaipuna.
Amesema mkakati huo uliweka msisitizo katika kumweka mteja katikati ya biashara, kuongeza ufanisi wa huduma, kupanua ujumuishaji wa kifedha na kuimarisha mchango wa benki katika maendeleo ya taifa.
Katika kipindi hicho, NMB ilieleza kuwa imeelekeza zaidi ya Sh.trilioni 28 katika sekta za kimkakati za uchumi, imelipa zaidi ya Sh. bilioni 700 kama gawio kwa wanahisa, imechangia Sh. trilioni 2.7 katika kodi kwa Serikali na kuwekeza Sh.bilioni 24 katika miradi ya maendeleo ya jamii.


Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema mchango wa taasisi za fedha kama NMB ni muhimu katika kukuza uchumi, kuimarisha sekta binafsi na kupanua ushiriki wa wananchi katika uchumi rasmi.
“Historia ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukikua kwa wastani wa takribani asilimia sita, haiwezi kutenganishwa na mchango wa taasisi kama NMB,” amesema Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake, Yonazi amesema hatua inayofuata ya ukuaji wa NMB itaendelea kuendana na mahitaji ya uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji katika teknolojia, huduma endelevu za kifedha, biashara ndogo na za kati pamoja na sekta zinazochochea ajira.
Amesema; “Kadiri nchi inavyokua na kubadilika, wajibu wetu ni kuhakikisha tunaendelea kutoa suluhisho za kifedha, uwekezaji na ubia unaohitajika kuunga mkono mageuzi hayo”.
Ameongeza kuwa mafanikio ya miaka mitano iliyopita yameiweka NMB katika nafasi nzuri ya kuendelea kuchangia safari ya Tanzania kuelekea uchumi shindani, jumuishi na endelevu unaolengwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.





