Aliyekuwa kiungo wa Yanga SC, Khalid Aucho, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Singida Black Stars, amemkaribisha rasmi kiungo mpya wa Yanga SC, Allan Okello, kufuatia kutambulishwa kwake kama mchezaji mpya wa klabu hiyo kongwe nchini.
Kupitia ukurasa rasmi wa Instagram wa Yanga SC, ambapo picha ya utambulisho wa Allan Okello iliwekwa hadharani, Khalid Aucho aliacha ujumbe maalum wa kumtakia heri kiungo huyo mpya, akionesha furaha, upendo na imani kubwa aliyonayo juu ya uwezo wake.
Aucho aliandika ujumbe huo akisema:

“Welcome to the best my little brother, may Allah bless you more and more and show them your magic. I am proud of you brother.”
Ujumbe huo kwa tafsiri ya Kiswahili una maana kuwa:
“Karibu katika klabu bora mdogo wangu, Mwenyezi Mungu akubariki zaidi na zaidi na awaonyeshe uwezo wako. Ninajivunia wewe kaka.”
Ujumbe wa Khalid Aucho unaonesha wazi mshikamano wa wachezaji wa zamani na wapya wa Yanga SC, pamoja na imani kubwa aliyonayo kuwa Allan Okello atakuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho. Ikumbukwe kuwa Aucho aliwahi kuvaa jezi la Yanga SC na kuacha alama katika safu ya kiungo kabla ya kujiunga na Singida Black Stars, hivyo maneno yake yana uzito mkubwa kutokana na uzoefu wake ndani ya klabu hiyo.
Ujio wa Allan Okello Yanga SC umeendelea kuvuta hisia za mashabiki na wadau wa soka nchini, wengi wakitarajia kuona ubora na ubunifu wake ukiisaidia Yanga katika mashindano ya ndani na kimataifa msimu huu.




