HomeHabariDAWASA yaimarisha ufuatiliaji wa Mto Ruvu kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika

DAWASA yaimarisha ufuatiliaji wa Mto Ruvu kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeongeza mikakati ya kuhakikisha uimarikaji wa huduma, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa vyanzo vya maji, ili kuhakikisha huduma ya majisafi inaendelea kuwa ya uhakika kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, ametembelea na kukagua hali ya Mto Ruvu katika eneo la Kitomondo Mkoani Morogoro kwa lengo la kutathmini mwenendo wa kiwango cha maji katika chanzo hicho kwa sasa ikilinganishwa na kipindi cha mvua za masika.

Ziara hiyo imelenga pia kujiridhisha kuhusu hali ya chanzo hicho muhimu cha maji kinachohudumia zaidi ya asilimia 87 ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na kutathmini maandalizi ya Mamlaka katika kutathimini na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza pindi kiwango cha Maji kitakapopungua.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhandisi Bwire amesisitiza umuhimu wa kuanza mara moja kutekeleza hatua za dharura na mikakati ili kuhakikisha mabadiliko ya kiwango cha maji katika Mto Ruvu hayaathiri upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi.

Amesema ufuatiliaji wa karibu wa hali ya vyanzo vya maji ni muhimu katika kuwezesha Mamlaka kuchukua hatua mapema na kupanga namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

DAWASA imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha huduma ya maji inakuwa endelevu kwa kuimarisha ufuatiliaji wa vyanzo vya maji na kuchukua hatua za mapema dhidi ya changamoto zinazoweza kuathiri upatikanaji wa huduma.

Mto Ruvu ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maji vinavyotegemewa katika utoaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo yanayohudumiwa na DAWASA.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments