HomeBiasharaPolisi wakamata watuhumiwa wawili kwa kutorosha mifugo 254 kwenda nje kwa magendo

Polisi wakamata watuhumiwa wawili kwa kutorosha mifugo 254 kwenda nje kwa magendo

Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU), kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili waliokuwa wakijaribu kutorosha mifugo 254 kwenda nchi jirani kwa njia ya magendo.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini (STPU), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika Kijiji cha Olkesumet, Kata ya Sinonik, Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, wakiwa na ng’ombe 70 pamoja na mbuzi na kondoo 184.

Kamanda Pasua amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

Aidha, amewataka wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo nchini kuzingatia sheria na taratibu za usafirishaji wa mifugo, akisisitiza kuwa ulipaji wa ushuru wa usafirishaji, hususan kwa mifugo inayovushwa kwenda nje ya nchi, ni wajibu wa kisheria na si hiari.

Pia ametoa wito kwa wananchi, hasa wanaoishi maeneo ya mipakani, kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyohusisha mifugo, ikiwemo utoroshaji kwa njia ya magendo.

Amesema vitendo vya utoroshaji wa mifugo vinaikosesha Serikali mapato, vinakiuka taratibu za usafirishaji na vinaweza kuathiri ustawi wa sekta ya mifugo, hivyo ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kukabiliana na uhalifu huo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments