Monday, May 18, 2026
spot_img
HomeElimuSerikali yataka vijana wapewe mwongozo wa taaluma za kusomea

Serikali yataka vijana wapewe mwongozo wa taaluma za kusomea

Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Kituye amesema vijana wanahitaji  mwongozo sahihi wa taaluma ili waweze kuchagua masomo ambayo wanayaweza na mahitaji ya soko la ajira.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kusaini makubaliano ya kushirikiana kutoa mwongozo kwa wanafunzi baina ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu DUCE na Wakala wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL).

Makubaliano hayo yalisainiwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam baina ya  Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Abdulmalik Mollel na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa  Pendo Malangwa.

KItuye alisema kwa kuzingatia hilo, ni jambo la faraja kuona kuwa DUCE pamoja na Global Education Link wameamua kuunganisha nguvu katika eneo hili muhimu la kuwapa mwongozo vijana.

 “Kwa niaba ya Ofisi ya Elimu Mkoa wa Dar es Salaam napenda kuupongeza tena uongozi wa DUCE pamoja na Global Education Link kwa kuanzisha ushirikiano huu muhimu. Ni Imani yangu kuwa hatua hii ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika namna tunavyowaandaa vijana wetu kwa elimu, ajira, ubunifu, na maisha ya baadaye,” alisema.

 “Nitumie fursa hii kuwapongeza sana DUCE pamoja na Global Education Link kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kusaidia maendeleo ya elimu na maandalizi ya vijana wetu kwa maisha ya kazi baada ya hatua mbalimbali za masomo,” alisema Kituye.

Mkurugenzi Mkuu wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel alisema  GEL imefikisha miaka 19 katika kufanyakazi ya kuwapa wanafunzi mwongozo wa taaluma za kusomea.

Alisema kazi kubwa ambazo wanafanya ni kuwatafutia wanafunzi wa Tanzania kupata fursa za kusoma nje ya nchi na kusaidia ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya ndani nan je ili kuchukua teknolojia kwenye nchi hizo.

Alisema nchi zilizoendelea zimefika hapo kutokana na maarifa makubwa ya wananchi wake hivyo GEL imeona umuhimu wa kuchukua maarifa hayo yaje kusaidia hapa nchini Tanzania.

Alisema GEL imesaini mikataba kama hiyo na vyuo vikuu vya Dodoma, Mzumbe, Nelson Mandela, TIA na vingine na kwamba kusaini na DUCE ni mwendelezo wa utaratibu huo.

“Kila chuo tunachosaini makubaliano tunakuwa na malengo maalum nacho, leo tumesaini na DUCE kwaajili ya mwongozo kwa wanafunzi na hatuishii kwa wanafunzi, wazazi ambao wanataka kujiendeleza kielemu au walimu wanaotaka kujiendeleza tunawapa mwongozo,” alisema Mollel.

Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa  Pendo Malangwa alisema tukio hilo linaonyesha dhamira ya dhati ya kuwaaandaa vijana kwenye maisha ya taaluma na hatimaye ajira siku za baadae.

Alisema kupitia ushirikiano huo wanafunzi wa chuo hicho watapata mwongozo wa kitaaluma na kuelewa fursa zilizoko ndani nan je ya nchi kwaajili ya kupambana na ushindani unaokua kwa kasi ulimwenguni kwenye soko la ajira.

Alisema DUCE inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kutoa elimu bora, kufanya tafiti na kuandaa wataalamu na kwamba GEL itaweka uzoefu wake kwa kuwaunganisha vijana kwa kuwapa ushauri na maendeleo ya kitaaluma.

Tunatarajia kuongeza mwongozo wa kitaaluma na ushirikishwaji wa wanafunzi na kuwajengea uwezo na kuimarisha mawasiliano kupitia vyombo vya habari ili kusaidia vijana kuelewa taaluma mbalimbali na mahitaji ya soko la ajira.

“Sote ni mashahidi hapa vijana wengi wakimaliza kidato cha sita hawana uwezo wa kuchagua wanachotaka kusoma, wengine wanachagua tu kwasababu walisikia, sasa kupitia ushirikiano huu tunataka vijana wachague kitu wanachokijua kitakacholeta tija kwenye maisha yao ya baadae,” alisema

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments