Monday, December 8, 2025
spot_img
HomeHabariPolisi kuchunguza mabweni kuungua Sumve Sekondari

Polisi kuchunguza mabweni kuungua Sumve Sekondari

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza likishirikiana na mamlaka nyingine za Serikali limeanza uchunguzi wa tukio la moto lililotokea Novemba 20, 2025, majira ya saa 7:13 mchana katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Sumve, iliyopo Kitongoji cha Sumve, Kata ya Sumve, Tarafa ya Ngula, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa, moto huo ulizuka wakati wanafunzi wakiwa madarasani na kuteketeza mabweni mawili ya wasichana yanayojulikana kama Nkwame na Dkt. Magufuli.

Inadaiwa kuwa moto ulisambaa kwa kasi kutokana na uwepo wa vifaa vinavyowaka haraka kama magodoro, nguo, mablanketi na mali nyingine za wanafunzi waliokuwa wakiishi katika mabweni hayo. Hata hivyo, hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa na chanzo cha tukio bado kinachunguzwa.

Mara baada ya mlipuko huo wa moto, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti kabla haujasababisha madhara makubwa zaidi. Baadhi ya mali zikiwemo magodoro, matranka, mablanketi, ndoo za maji na viatu ziliokolewa.

Kwa sasa, uchunguzi wa chanzo cha moto huo unaendelea huku ulinzi ukiimarishwa katika shule hiyo na shule jirani kwa ushirikiano wa wananchi pamoja na uongozi wa shule.

Kamanda Mtafungwa ametoa wito kwa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kubaini chanzo cha tukio hilo kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kufanikisha uchunguzi huo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments