Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, ameitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha ujenzi wa jengo la ofisi hiyo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma bora.
Prof. Kabudi ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lililopo Mtaa wa Kilimani, jijini Dodoma.
Amepongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kuhakikisha jengo linakamilika kwa wakati na kuanza kutumika.

“Ujenzi wa Ofisi za Umma lazima ujengwe kwa hadhi na uakisi matarajio ya muda mrefu ujao kulingana na mahitaji ya Ofisi. Niwapongeze kwa kuzingatia hilo katika ujenzi wa jengo lenu,” amesema Prof. Kabudi.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu Fransis Mutungi, amemshukuru Prof. Kabudi kwa maelekezo aliyoyatoa na kusema Ofisi hiyo ina mpango wa kuajiri na kuwa na watendaji wenye taaluma mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa sayansi ya siasa na elimu ya jamii.


Amesema wataalamu hao watasaidia kufanya tafiti, kuchakata taarifa na kutoa miongozo kulingana na mabadiliko na mahitaji ya kisiasa nchini.
“Taasisi hii ni kitovu cha mambo ya siasa. Tunahitaji wataalamu wenye ujuzi tofauti watakaosaidia katika kufanya tafiti na kutoa taarifa zenye weledi zitakazosaidia taasisi kufanya kazi vizuri zaidi,” amesema Jaji Mstaafu Mutungi.
Awali, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Magohu Zonzo, amesema ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa na Kampuni ya Group Six International na unasimamiwa na mshauri elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi kupitia kampuni tanzu ya ARU, kwa ajili ya usanifu na usimamizi wa mradi.






