Tuesday, March 3, 2026
spot_img
HomeElimuWizara ya Elimu yataka ushirikiano kuimarisha huduma ya chakula na lishe mashuleni

Wizara ya Elimu yataka ushirikiano kuimarisha huduma ya chakula na lishe mashuleni

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka taasisi za kimataifa na wadau wa maendeleo kuongeza ushirikiano katika kuboresha miradi ya chakula na lishe mashuleni, ili kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora na mazingira rafiki ya kujifunzia.

Akizungumza jana, Desemba 1, 2025 jijini Dar es Salaam katika kikao cha wadau wa mpango wa chakula shuleni, Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji Sera za Elimu Msingi, Victor Bwindiki, alisema kikao hicho kimeandaliwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kuchambua mafanikio, changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha huduma ya chakula mashuleni.

“Kila mshiriki amepata fursa kueleza mbinu bora, masomo tuliyojifunza pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza, na kujadili namna ya kukabiliana nazo ili kuboresha mpango wa chakula shuleni nchini,” alisema Bwindiki.

Aidha, Bwindiki alilishukuru Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kuendelea kushirikiana na serikali kupitia msaada wa kitaalamu na kifedha ambao umechangia kuimarika kwa mpango wa lishe mashuleni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Lishe, VVU na Mipango ya Shuleni kutoka WFP, Vera Kwara, aliipongeza serikali pamoja na wadau kwa jitihada wanazoendelea kufanya katika kuendeleza mpango huo muhimu kwa ustawi wa elimu nchini.

“Kwa baadhi ya watoto, mlo wa shule ndio chakula chenye lishe kamili wanachokipata kwa siku. Kuongeza utofauti wa vyakula, hususan vile vyenye protini na virutubisho, ni hatua muhimu kwa afya na ukuaji wao,” alisema Vera.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments