Kampuni ya CRDB Insurance Company imetangaza kupata faida ya shilingi bilioni 4.4 baada ya kodi kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2025 ikipanda kutoka faida ya shilingi milioni 343.1 iliyopata mwaka 2024.
Kutokana na mafanikio hayo, Bodi ya Wakurugenzi imependekeza kutoa gawio la shilingi 439 kwa kila hisa, sawa na jumla ya shilingi bilioni 1.5, huku ikionyesha imani ya kupata matokeo bora zaidi katika mwaka 2026.
Katika kipindi hicho, Kampuni ilikusanya michango ya wateja waliokata bima (Gross Written Premium) yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 55.7, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa mwaka uliopita, ukuaji uliochangiwa na huduma zilizotolewa kwa wateja wa bima ya magari, dhamana ya mikopo na bima ya moto ukiungwa mkono na mikakati madhubuti ya usambazaji na kuongezeka kwa soko.




Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Company, Wilson Mnzava anasema: “Matokeo haya yanaakisi uimara wa biashara yetu ya msingi, ufanisi wa mikakati yetu ya usambazaji pamoja na dhamira yetu ya kutoa thamani kwa wateja. Tumeimarisha uwezo wetu wa kuhudumia na kutumia teknolojia kuongeza ufanisi na kukidhi mahitaji na matarajio ya mteja wetu. Tukijenga juu ya mafanikio haya, tuna imani ya kupata matokeo bora zaidi mwaka 2026.”
Pamoja na kupendekeza gawio la shilingi 439 kwa kila hisa, Bodi imeshauri sehemu ya faida iliyopatikana itumike kuimarisha mtaji na kusaidia mipango ya upanuzi wa biashara siku zijazo.





Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Insurance Company, Omary Mwaimu amesema mafanikio yaliyopatikana yanaonyesha ukubwa wa ukuaji na ubora wake, ukiungwa mkono na misingi imara ya uongozi na usimamizi.
“Ukuaji mkubwa wa michango ya bima, faida na mtaji unaonyesha ufanisi wa mkakati wetu na nidhamu ya utekelezaji wake. Bodi tunaendelea kujikita katika kudumisha kasi hii ya ukuaji huku tukilinda maslahi ya muda mrefu ya Kampuni na wadau wake,” anasema Mwaimu.





