Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuanza kwa operesheni maalum ya kusaidia meli zilizokwama katika malango wa Hormuz, akieleza kuwa ni msaada wa kibinadamu kwa mataifa yasiyohusika moja kwa moja na vita.
Amesema operesheni hiyo inaanza rasmi Jumatatu, ikilenga kusaidia meli na wafanyakazi waliokwama kwa zaidi ya miezi miwili kufuatia vizuizi vya Iran katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Trump ameongeza kuwa Marekani itaziongoza meli hizo kupita salama, huku akionya kuwa jaribio lolote la kuingilia operesheni hiyo litajibiwa kwa nguvu.
Hatua hiyo inakuja wakati mvutano ukiendelea kati ya Marekani, Israel na Iran, huku Tehran ikithibitisha kupokea majibu ya pendekezo lake la amani, lakini ikisema bado inalichambua.
Hata hivyo, Trump ameonyesha kutoridhishwa na pendekezo hilo, wakati Iran ikisisitiza kuwa haitarejea kwenye mazungumzo ya nyuklia hadi vita vitakapomalizika.




