Zaidi ya waumini 100 wa Kanisa Katoliki leo wamefika katika Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania na kuwasilisha barua rasmi yenye malalamiko dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Ruwa’ichi, pamoja na Padri Charles Kitima.
Barua hiyo, ambayo ilikabidhiwa kwa njia rasmi ya kidiplomasia katika Ubalozi wa Vatican mkoani Dar es Salaam, ina madai mbalimbali ikiwamo ukiukwaji wa maadili ya uongozi wa Kanisa, matumizi mabaya ya mamlaka ya kiroho, pamoja na matumizi ya lugha zinazodaiwa kuwavunjia heshima waumini wa Kanisa.
Hivi karibuni kumekuwa na mvutano ndani ya Kanisa Katoliki, ambapo baadhi ya waumini wamejitokeza hadharani wakipinga misimamo ya viongozi wao. Waumini hao wanadai kuwa viongozi hao wamejikita zaidi kwenye masuala ya siasa badala ya kuzingatia na kusimamia maadili na mafundisho ya vitabu vitakatifu vya Kanisa.
Madai haya yameibua mjadala mpana ndani ya jamii ya waumini, huku viongozi wa Kanisa wakilazimika kutoa majibu na maelezo juu ya malalamiko haya yanayohusiana na uongozi na uwajibikaji wao.




