Friday, February 13, 2026
spot_img
HomeAfyaWaziri Dk. Gwajima azindua mkakati wa kitaifa wa kisekta wa kutokomeza ukeketaji

Waziri Dk. Gwajima azindua mkakati wa kitaifa wa kisekta wa kutokomeza ukeketaji


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amezindua Mkakati wa Kitaifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji Nchini (2025/2026–2029/2030) katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji yaliyofanyika Februari 12, 2026, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.

Uzinduzi huo unalenga kuimarisha juhudi za kitaifa za kulinda haki, afya na ustawi wa wanawake na watoto wa kike pamoja na kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya mila na desturi hatarishi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Gwajima amesema mkakati huo utaimarisha uratibu na ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla ili kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukeketaji. Amebainisha kuwa mikoa ya Arusha na Manyara bado ina viwango vya juu vya ukeketaji, hali inayohitaji hatua madhubuti, ushirikiano wa karibu na ushiriki wa kila mdau.

Amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanaume katika mapambano hayo kwa kuwapatia elimu, akieleza kuwa mara nyingi wao ni wahamasishaji wakuu wa vitendo hivyo. Katika kuonesha msimamo huo, Dk. Gwajima aliongoza maandamano ya wanaume kama ishara ya kupinga ukeketaji na kuhamasisha jamii kubadili mitazamo.

Aidha, ametoa shukrani kwa wadau mbalimbali wanaoisaidia Serikali katika juhudi hizo, wakiwemo Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), C-SEMA, SOS Children’s Village, Compassion International Tanzania pamoja na mashirika mengine ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Kimathi, amemshukuru Waziri kwa kuichagua Monduli kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo, akisema hatua hiyo imeongeza ari na mwamko mpya katika vita dhidi ya ukeketaji. Ameahidi kuwa Wilaya itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

Naye Katibu wa Viongozi wa Mila Wilaya ya Monduli (Laigwanan), Natuli Letema, amesema viongozi wa mila wako tayari kushirikiana na Serikali ya Mkoa katika kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia na ukeketaji. Ameongeza kuwa ari mpya iliyoamshwa itasaidia jamii kubadilika na kuweka mbele ustawi na ulinzi wa watoto wa kike.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments