Upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wasio na uwezo nchini sio changamoto tena, baada ya kuanza rasmi kwa kitita cha huduma muhimu chini ya mpango wa bima ya afya kwa wote.
Kupitia kitita hicho, makundi ya wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu yatanufaika kwa kuchangia Sh150,000 pekee kwa mwaka, kiasi kitakachohudumia kaya yenye watu wasiozidi sita.
Hata hivyo, kuanza kwa kitita hicho ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, alipoahidi ndani ya siku 100, atazindua Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na makundi maalumu yatakuwa ya kwanza kunufaika.

Taarifa iliyotolewa leo, Jumatano Februari 25, 2026 na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, imeeleza kaya itanufaika ikiwa na mwanachama mchangiaji, mwenza wake na wategemezi wanne, wakiwemo mzazi wa mwanachama au wa mwenza wake, mtoto wa kuzaa, kuasili au wa kambo aliye chini ya miaka 21, au ndugu wa damu mwenye umri chini ya miaka 21.
Katika kitita hicho kinachoanza rasmi kesho Februari 26, wanachama watapata huduma za usajili, kulazwa katika wodi za kawaida, ushauri wa madaktari na maofisa afya, pamoja na vipimo 80 vya maabara na radiolojia kama damu, mkojo, malaria, kisukari, VVU, X-Ray na ultrasound.
Aidha, watapatiwa dawa na vifaa tiba 247 kwa magonjwa ya kawaida, sugu na dharura, pamoja na huduma 36 za upasuaji mdogo na mkubwa, ikiwemo uzazi, mimba nje ya kizazi, hysterectomy, laparotomy na kujifungua kawaida.




