Baada ya miaka kadhaa ya kukaa darasani pamoja na kufanya utafiti, hatimaye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela amehitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini yaani the University of South Africa (UNISA).
Dk. Nsekela ametunukiwa shahada hiyo ya juu baada ya kufanya utafiti wenye kichwa cha habari kisemacho: “Corporate governance and financial performance of East African banks: The moderating role of information leakage” kwa tafsiri isiyo rasmi ikimaanisha “Usimamizi wa makampuni na ufanisi wa kifedha wa benki za Afrika Mashariki: Jukumu la kudhibiti uvujaji wa taarifa.”
Mafanikio haya ya kitaaluma yanaakisi mtazamo wa uongozi unaojengwa juu ya kujifunza kila siku, utambuzi wa kimkakati, na ubunifu endelevu, misingi iliyotambulisha uongozi wa Dkt. Nsekela tangu alipoteuliwa kuiongoza Benki ya CRDB Oktoba 2018.




‘Usimamizi makini wa makampuni kama utafiti wangu unavyoonyesha, si jambo la nadharia bali ni msingi wa utendaji bora na mafanikio endelevu ya kifedha na kujenga imani ya taasisi za fedha ndani ya ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Safari hii ya kitaaluma imetokana na msukumo wa udadisi pamoja na ukuaji endelevu,” amesema Dk. Nsekela.
Dkt. Nsekela amewashukuru maprofesa na walimu wa UNISA kwa maelekezo, usimamizi wa kitaaluma na miongozo mbalimbali waliyokuwa wanampa kwa kipindi chote cha masomo yake ambayo imemwezesha kuhitimu shahada yake ya uzamivu. Vilevile ameishukuru familia yake kwa uvumilivu waliounyesha kwa kipindi hicho ambacho alilazimika kusafiri kila mara kutokana na ratiba ngumu aliyokuwa nayo.

“Kwa wkaurugenzi wenzangu na maafisa watendaji wakuu nchini Tanzania na afrika kwa ujumla, napenda kuwakumbusha kwamba kujifunza ni suala endelevu. Yatupasa kutenga muda wa kujifunza maarifa na ujuzi mpya utakaoimarisha uongozi wetu, kuboresha uamuzi tunaoufanya na kuchangia ufanisi zaidi wa taasisi zetu,” amesihi Dkt. Nsekela.
Akizungumza katika hafla ya mahafali hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori amempongeza Dkt. Nsekela anayetajwa kama mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi wa makampuni ya fedha barani Afrika, akibainisha uwiano mkubwa kati ya utafiti wake wa kitaaluma na falsafa za uongozi wake wa kila siku ndani ya Benki.
”Dk. Nsekela ameifanya Benki ya CRDB kuwa kiongozi katika ufanikishaji na uwezeshaji biashara hivyo kiwezesha kutambuliwa na GCF (Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa) katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Utafiti wake unaonyesha ni jinsi gani usimamizi makini wa kampuni au shirika na udhibiti wa uvujaji hovyo wa taarifa unavyoimarisha ufanisi wa utendaji, mambo yanayodhihirika kwa uwazi ndani ya Benki ya CRDB,” amesema Profesa Mori.
Mwenyekiti amefafanua zaidi kwamba mafanikio ya Dkt. Nsekela yanadhihirisha ubora wa kitaaluma ulivyo na mchango katika uongozi wa taasisi za kibiashara. “Safari yake inaonyesha kuwa mafanikio ya kitaaluma na utendaji makini vinategemeana kwa kiasi kikubwa. Mafanikio ya Benki ya CRDB ni mfano halisi wa jinsi utawala bora, uongozi makini na kujifunza kila siku ni mambo yanayoweza kuibadilisha taasisi ikawa bora zaidi,” amesema.








