Friday, February 27, 2026
spot_img
HomeBiasharaNMB yatoa Sh bilioni 12.4 kwa wafanyabiashara

NMB yatoa Sh bilioni 12.4 kwa wafanyabiashara

Jumla ya shilingi 12.4 bilioni zimetolewa na NMB Bank kwa zaidi ya wafanyabiashara 6,011, ambapo wanufaika pia wamepewa elimu ya fedha na uongozi.

Takwimu hizo zimetolewa na Meneja Mwandamizi wa Idara ya Biashara za Serikali, Amanda Feruzi, kwenye mkutano wa Jumuiya ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Ukanda wa Ziwa Victoria (LVRLAC) unaoendelea katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma. Fedha hizo ni sehemu ya shilingi 13 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa NMB kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu katika mfumo wa majaribio kwenye Halmashauri sita.

Halmashauri zilizochaguliwa ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa ya Songea, na Halmashauri za Newala, Bumbuli na Itilima. Feruzi amesema NMB ipo tayari kushirikiana na Jumuiya hiyo kama ilivyokuwa na ushirikiano wa kifedha na kufadhiri mikutano yao kila mwaka.

Amesema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika miradi ya uwezeshaji wananchi, ikitumia ujuzi wake katika APF (African Project Finance) na kuwekeza katika teknolojia na bidhaa za kifedha, ikiwa benki ya kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kutoa hati fungani za Jinsia (Jasiri Bond) na Uendelevu (Jamii Bond) zilizovutia wawekezaji wa ndani na nje katika masoko ya mitaji ya kimataifa.

Feruzi pia alifafanua kuwa NMB ilikuwa benki ya kwanza kuunganishwa katika mfumo wa GePG, ikichangia ukusanyaji mkubwa wa mapato na kubuni suluhisho kwa wateja na Serikali. Amehimiza wajumbe 42 kutoka mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera kutumia fursa ya Serikali kutafuta mitaji kutoka kwa wawekezaji ili kuzalisha vyanzo vipya vya mapato, huku akisisitiza kushirikiana na sekta binafsi kupitia uwekezaji kwa njia ya PPP na APF.

Manufaa yanayotarajiwa kutokana na uwekezaji huo ni pamoja na: maboresho ya miundombinu kwa haraka, kupunguza utegemezi kwenye bajeti kuu, utekelezaji wa miradi mara moja, na kutumia uzoefu wa sekta binafsi katika kupata mitaji.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi), Reuben Kwagilwa, amewataka Wakurugenzi kote nchini kushirikiana na sekta binafsi na kutumia huduma za kifedha za NMB. Pia alisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika kuchezwa au kuchelewesha matumizi ya fedha.

“Wakurugenzi, lipeni madeni ya Jumuiya kwa wakati ili mjiendeshe vyema na mfanikishe mipango yenu kwa kushirikiana na NMB,” amesema Kwagilwa, akiwataka pia kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua kwa wakati badala ya kusubiri viongozi wa juu kuwasikiliza.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments