Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), inatarajia kuanzisha kiliniki maalum ya uchunguzi wa magonjwa ya saratani kwa wanawake pekee hospitalini hapo mwishoni mwa mwaka huu ili kuwarahishia kugundua mapema ugonjwa huo.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Delilah Kimambo, wakati akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na Chama cha Madaktari Biongwa Wanawake wa Figo (NESOT).
“Kwa kutumia kliniki hii tunatarajia kugundua mapema saratani zinazowakabili wanawake ili waweze kuhudumiwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” alisema Dk Delilah
Alisema kliniki za saratani ni chanche nchini hivyo wagonjwa wengi hasa wanawake wamekuwa wakigundua saratani zikiwa kwenye hatua ambayo haitibiki hivyo kuanzishwa kwa kliniki hiyo kutakuwa na msaada mkubwa kwa wanawake kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya mapema.
“Tunaamini tukifanya hivi tutapunguza matatizo ya wanawake kwasababu watachunguzwa mapema na kupata tiba mapema na kauli mbinu yetu Muhimbili mwaka huu tunakwenda kuboresha afya ya mwanamke na tutafanya hivyo kwa vitendo,” alisema Dk Delilah
Alisema NESOT ni chama cha madaktari ambacho kina wanawake wabobezi kwenye maradhi ya figo ambao wamekua na msaada mkubwa kwenye tiba hiyo hapa nchini


Dk Kimambo alisema kuna wagonjwa 3,000 mpaka 4,000 wanafanya matibabu ya kuchuja damu kila mwaka na wengine wanashindwa kuhudhuria kliniki kwa kushindwa kugundulika mapema
Alisema kuna wanawake wanakwenda kujifungua lakini wanapata maradhi ya figo wakati wa kujifungua akisema kuwa Muhimbili imejipanga kuhakikisha wanawake wanaokwenda kujifungua hawapati maradhi ya figo na wanajifungua salama kwani watafanyiwa uchunguzi wa mapema
“Kundi la wanawake wajawazito tunaliangalia sana kuhakikisha wanapata huduma mapema wasiharibu figo zao, mama ni nguzo ya maisha hawezi kwenda kujifungua halafu aishie kupata maradhi ya figo kwa hiyo tutawaangalia sana wasipate maradhi hayo wakati wa kujifungua,” alisema
Alisema kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii nzima kuhusu namna bora ya kulinda afya ya mama na mtoto ili kuhakikisha wanapokwenda kujifungua wanajifungua salama bila kupata athari za figo.

Alisema kuna matatizo mengine yanayosababishwa na ugonjwa wa figo kama kisukari na shinikizo la damu ambayo huwa yanawashambulia wanawake.
“Tunawaelimisha wanawake wafanye mazoezi, wale kwa afya, wasitumie chumvi nyingi watumie mboga mboga za majani zaidi kuliko wanga na wapunguze uzito kwani uzito uliopitiliza ni chanzo cha magonjwa mengi yanayosababisha madhara kwenye figo,” alisema
“Tunaamini mwanamke akiwa na afya bora jamii yote itakuwa na afya bora kwa hiyo mwishoni mwa mwaka huu tutakuwa na kliniki tatu moja maalum ikiwa ni hiyo ya saratani kwa wanawake pekee ili wasipate matatizo ya kuhalibu figo wanapokwenda kujifungua,” alisema
Naye Makamu wa Rais wa NESOT, Dk Sudakshina Ghosh ambaye ni daktari bingwa wa figo, alisema walisherehekea mafanikio ya wanawake wanaojihusisha na tiba ya figo.
“Tunapenda kuwatambua madaktari bingwa, wauguzi, madaktari wanafunzi ambao wote kwa pamoja wako kwenye mnyororo wa matibabu ya figo hapa nchini NESOT tunaona ni baraka kwetu kuwatambua wanawake hawa kwenye siku ya wanawake hawa,” alisema





