Wednesday, March 18, 2026
spot_img
HomeHabariMatumizi ya mtandao yachochea maendeleo ya uchumi, serikali yaendelea kupanua mawasiliano nchini

Matumizi ya mtandao yachochea maendeleo ya uchumi, serikali yaendelea kupanua mawasiliano nchini

Serikali imewataka wananchi kutumia huduma za mawasiliano na mtandao kwa manufaa ya kiuchumi ili kuchochea maendeleo binafsi na ya taifa, sambamba na juhudi zinazoendelea za kupanua miundombinu ya mawasiliano nchini.

Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika mnara wa mawasiliano uliopo Kata ya Kibada, ambapo ilielezwa kuwa uwekezaji katika sekta ya mawasiliano una lengo la kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angel Kairuki, amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wengi zaidi, ili kuwawezesha kutumia teknolojia katika kukuza biashara, elimu na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Amesema upanuzi wa huduma za mawasiliano unalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na masoko, jambo ambalo linasaidia kuongeza kipato kwa wananchi na kuimarisha uchumi wa taifa kwa ujumla.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Peter Mwasalyanda, amesema kuwa minara 758 yenye thamani ya shilingi bilioni 126 imejengwa katika mikoa yote 26 ya Tanzania, huku zaidi ya minara 304 ikiboreshwa kutoka teknolojia ya 2G hadi 4G ili kuongeza ubora wa huduma za intaneti.

Ameongeza kuwa mradi huo ulikamilika kwa asilimia 100 mwaka 2023 kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano, hatua iliyochangia kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa wananchi wengi zaidi.

Katika Kata ya Kibada, mnara wa mawasiliano uliogharimu shilingi milioni 89.75 unatoa huduma kuanzia 2G hadi 5G, na unahudumia zaidi ya wananchi 28,000 tangu ulipoanza kufanya kazi mwaka 2024.

Wananchi wa eneo hilo wameeleza kuwa uwepo wa mnara huo umefungua fursa mpya za kiuchumi. Mkazi wa Kibada, Daniel Shija, amesema huduma ya mtandao imewezesha kupanua biashara na kurahisisha mawasiliano ya kibiashara, huku pia ikisaidia wanafunzi kupata rasilimali za kujifunzia mtandaoni.

Naye Mboni Mohamed Mbegu ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za mawasiliano, akisema hatua hiyo imekuwa msaada mkubwa katika shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mitandao kwa maendeleo, akiwahimiza wananchi kuachana na matumizi yasiyofaa ambayo hayaleti tija kwa jamii.

Serikali inaendelea kusisitiza kuwa maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano ni nyenzo muhimu katika kujenga uchumi wa kidijitali unaowanufaisha Watanzania wote.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments