HomeHabariACT Wazalendo yaitaka serikali uchunguzi huru wa matukio ya uchaguzi

ACT Wazalendo yaitaka serikali uchunguzi huru wa matukio ya uchaguzi

Chama cha ACT Wazalendo kimepinga uamuzi wa Serikali kuunda Tume ya Rais ya kuchunguza matukio yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, kikisema muundo na hadidu rejea za tume hiyo haviwezi kujenga imani kwa waathirika, wananchi na jumuiya ya kimataifa.

Katika taarifa iliyotolewa Agosti 8, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, chama hicho kimesema kinatambua umuhimu wa uchunguzi kuhusu matukio hayo, lakini hakina imani kuwa tume iliyoundwa inaweza kufanya uchunguzi huru, usio na upendeleo na wenye uwezo wa kubaini ukweli na kuwawajibisha waliohusika.

ACT Wazalendo imedai kuwa Serikali, ambayo inatuhumiwa kushindwa kuzuia au kuhusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi huo, haiwezi kuwa chombo kinachounda, kuelekeza na kusimamia uchunguzi wa tuhuma zinazoihusu.

“Kanuni za haki zinataka mtuhumiwa achunguzwe na chombo huru, si kujichunguza mwenyewe,” imeeleza taarifa hiyo.

Chama hicho pia kimekosoa hadidu rejea za tume hiyo, kikidai kuwa zinaelekeza zaidi katika kuwatafuta na kuwachunguza watu wanaodaiwa kuhusika na vurugu, badala ya kuweka uzito unaostahili katika kuchunguza madai ya mauaji, majeruhi, watu kupotea na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na vyombo vya dola.

Kwa msingi huo, ACT Wazalendo kimesema tume hiyo inaonekana zaidi kuwa chombo cha kuilinda Serikali dhidi ya tuhuma zinazoiandama kuliko kuwa chombo cha kutafuta ukweli, kutenda haki na kuhakikisha uwajibikaji.

“Kwa sababu hizo, ACT Wazalendo haitambui Tume hii kama chombo kinachoweza kutoa uchunguzi unaoaminika,” imeeleza taarifa hiyo.

Chama hicho kimerejea wito wake wa kutaka kuundwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa utakaoendeshwa au kusimamiwa na taasisi zinazotambulika kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) au Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, uchunguzi huo unapaswa kulenga kubaini ukweli, kuwawajibisha wote waliohusika bila upendeleo na kuhakikisha waathirika wanapata haki.

Aidha, chama hicho kimeitaka Serikali kuwaachia huru wafungwa na watuhumiwa wote wa kesi zenye muktadha wa kisiasa, pamoja na kuwapatia waathirika msaada wa kitabibu, kisheria, kisaikolojia na kifedha.

ACT Wazalendo pia imetaka kuanza kwa dhati kwa mchakato wa Katiba Mpya pamoja na mageuzi ya kisiasa, ikisema hatua hizo ni muhimu katika kujenga taasisi huru na kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

Chama hicho kimesisitiza kuwa kitaendelea kusimama katika misingi ya “Ukweli, Haki na Uwajibikaji”, kikieleza kuwa amani ya kudumu haiwezi kujengwa kwa kuficha ukweli, bali kwa kuuweka wazi na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake bila upendeleo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments