Thursday, May 7, 2026
spot_img
HomeBiasharaBei mpya za vyombo vya majini yatikisa wananchi

Bei mpya za vyombo vya majini yatikisa wananchi


Wananchi wanaotumia usafiri wa baharini kati ya Zanzibar na Tanzania Bara wanatarajiwa kuanza kulipa nauli mpya za vyombo vya abiria kuanzia Mei 11 mwaka huu kufuatia ongezeko la bei ya tiketi lililotangazwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), hatua ambayo tayari imeanza kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wasafiri na wafanyabiashara wadogo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 6, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Mtumwa Said Sandal, nauli za daraja la kawaida (Economy) kwa baadhi ya vyombo vya mwendo kasi zimeongezeka kutoka shilingi 35,000 hadi 40,000 huku tiketi ya mtoto ikipangwa kuwa shilingi 20,000.

Mtumwa amesema sababu za ongezeko hilo ni kupanda kwa gharama za mafuta pamoja na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa vipuri kutoka nje ya nchi kuja Tanzania. 

“Kutokana na hali hiyo, ZMA inawataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuzingatia viwango vilivyopitishwa rasmi ili kuepusha usumbufu kwa wasafiri,” amesema Mtumwa.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza kuhusu ongezeko hilo wamesema hatua hiyo inaongeza ugumu wa maisha na kuathiri shughuli zao za kila siku.

Mariam Juma, mkaazi wa Kisauni, amesema licha ya serikali kueleza sababu za kupanda kwa gharama hizo, wananchi wa kipato cha chini ndio wanaobeba mzigo mkubwa kutokana na hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha.

Wakati huo huo, madereva wa daladala Zanzibar nao wameitaka serikali kuwafikiria kwa kuongeza bei ya nauli kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na vipuri vya magari.

Abdallah Mzee Abdallah, dereva wa daladala njia ya Nyamanzi hadi Darajani, amesema gharama za maisha zimekuwa kubwa huku kipato wanachopata hakikidhi mahitaji yao ya kila siku kutokana na nauli kubaki shilingi 800.

“Sisi Zanzibar tofauti na Tanzania Bara, wao bei zikiongezeka wanaandamana, lakini sisi huku hatuna tabia hiyo mpaka serikali iamue kuongeza bei. Tunaiomba serikali itufikirie na sisi,” amesema.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments