Balozi mteule wa Marekani nchini Tanzania, William Trachman, amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025, bado Tanzania inaendelea kuwa mshirika muhimu wa Marekani katika biashara, usalama na maendeleo ya kikanda.
Katika hotuba yake mbele ya Kamati ya Seneti ya Marekani, Trachman amesema matukio ya vurugu baada ya uchaguzi yameibua wasiwasi kuhusu mwelekeo wa Tanzania kama mshirika wa kuaminika, lakini anatambua hatua chanya ambazo Tanzania imeanza kuzichukua.
Amesema atakapothibitishwa kushika nafasi hiyo, atafanya kazi moja kwa moja na viongozi wa Tanzania, akiwemo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuendeleza maeneo ya ushirikiano yenye manufaa kwa pande zote na kusaidia utulivu wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, ameielezea Tanzania kuwa nchi muhimu kimkakati duniani kutokana na idadi ya watu zaidi ya milioni 65, urithi mkubwa wa tamaduni kutoka zaidi ya makabila 120 na utajiri wa rasilimali asilia.
Amesema kwa miongo mingi Tanzania na Marekani zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika afya, usalama na maendeleo ya uchumi, huku uhusiano huo ukijengwa katika msingi wa kuheshimiana na maslahi ya pamoja.




