📌Lengo ni kuunganisha Mkoa wa Kagera na Gridi ya Taifa
📌Zaidi ya bilioni 270 zitatumika kutekeleza mradi
Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Benaco, mradi unatarajiwa kuunganisha Mkoa wa Kagera katika Gridi ya Taifa.
Hafla hiyo imefanyika leo Mei 9, 2026 katika eneo la Benaco wilayani Ngara, mkoani Kagera, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, TANESCO pamoja na wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Ndejembi amesema Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya nishati kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 270 na utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 24.
“Leo tupo hapa kudhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika. Ili huduma ya umeme iwafikie wananchi hadi vitongojini, ni lazima kuwe na miundombinu imara ya kusafirisha na kupooza umeme,” amesema Ndejembi.
Aidha, amesema njia hiyo ya umeme yenye msongo wa kilovolti 220 ina uwezo mkubwa zaidi ukilinganisha na laini ya sasa ya kilovolti 132 inayopokea umeme kutoka nchini Uganda, hatua ambayo itaifanya Kagera kuingia rasmi katika Gridi ya Taifa na kuondoa changamoto za upatikanaji wa umeme mkoani humo.
“Tunatarajia ndani ya miezi 24 Mkoa wa Kagera uwe umeunganishwa katika Gridi ya Taifa na changamoto za umeme kwa wananchi ziwe historia,” amesema.





Pia, Waziri Ndejembi ameuagiza uongozi wa TANESCO kuhakikisha wananchi hawaendelei kusubiri huduma ya umeme kwa muda mrefu kwa kutafuta transfoma kubwa zitakazosaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea.
Sambamba na hilo, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati bila ucheleweshaji, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa ajira kwa wananchi wa maeneo husika pamoja na kulipa fidia stahiki kwa waliopisha utekelezaji wa mradi.
“Niwatake wakandarasi kukamilisha mradi huu kwa wakati bila ucheleweshaji wowote. Vilevile, hakikisheni wananchi wanapata ajira kupitia utekelezaji wa mradi huu pamoja na kulipwa fidia zao kwa wakati,” amesema Ndejembi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema mradi huo umetengewa jumla ya dola za Marekani milioni 105.6, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 279 za Kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo miwili.




Amesema hadi sasa wakandarasi wote wameshalipwa malipo ya awali ili kuanza kazi, huku zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi likiendelea ambapo zaidi ya shilingi bilioni 1.7 tayari zimetolewa katika awamu ya kwanza.
Bw. Twange amesema maeneo ya Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini pamoja na Manispaa ya Bukoba kwa sasa yanapata umeme kutoka nchini Uganda kupitia laini ya kilovolti 132 kutoka Masaka hadi Kituo cha Kupooza Umeme cha Kyaka.
“Mradi huu utaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kusaidia kukuza shughuli za kiuchumi na uzalishaji katika Mkoa wa Kagera.
TANESCO imejipanga kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika kwa wakati,” amesema Bw. Twange.
Naye Mjumbe wa Bodi ya TANESCO, Bi. Zuhura Bundala, ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wizara ya Nishati kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Amesema mradi huo utafungua fursa mbalimbali za maendeleo kwa wananchi wa Kagera kupitia ongezeko la shughuli za uzalishaji mali, ajira kwa vijana pamoja na kuinua kipato cha wananchi.
“Mradi huu utafungua fursa nyingi za maendeleo kwa wananchi wa Kagera kwa kuongeza shughuli za uzalishaji mali, ajira kwa vijana pamoja na kuinua uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema Bi. Bundala.
Kwa niaba ya Bodi ya TANESCO, ameahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Bw. Mathias Kahabi, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Nishati kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo ya umeme wilayani humo.
Amesema katika Jimbo la Ngara vijiji vyote 75 tayari vimefikiwa na huduma ya umeme, huku vitongoji 219 kati ya vitongoji 389 vikiwa tayari vimeunganishiwa umeme.
Akihitimisha hafla hiyo, Waziri Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya nishati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na ya uhakika.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika miradi ya umeme ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na mazingira bora ya kufanya shughuli za maendeleo. Mradi huu ni mwanzo wa mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa Mkoa wa Kagera,” amesema Ndejembi.




