Walipakodi wakubwa nchini wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuboresha huduma zake, ikiwemo kuwafikia katika maeneo yao ya kazi na kusikiliza changamoto zinazowakabili, hatua waliyosema imeimarisha ushirikiano na kujenga mazingira rafiki ya ulipaji kodi.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Agosti 13, 2026, jijini Dar es Salaam, baada ya Idara ya Walipakodi Wakubwa ya TRA kufanya ziara katika baadhi ya taasisi na kampuni kwa lengo la kusikiliza changamoto, kupata maoni na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika huduma za kodi.
Naibu Kamishna wa Operesheni kutoka Idara ya Walipakodi Wakubwa TRA, Eva Raphael, amesema Alhamisi imetengwa kwa ajili ya kuwasikiliza walipa kodi, ikiwa ni sehemu ya mpango ulioanzishwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda.




Amesema ziara hizo pia zinatumika kuwashukuru walipa kodi kwa ushirikiano wao na kutambua mchango wao katika kuhakikisha Serikali inapata mapato.
Eva amesema TRA itaendelea kuwa karibu na walipa kodi ili kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi kwa wakati.
Mkurugenzi wa Fedha wa HTT Franco Tanzania, Ruben Sarumbu, amesema hatua ya TRA kuwafikia walipakodi imeleta mabadiliko katika uhusiano kati ya Mamlaka hiyo na wafanyabiashara.



Sarumbu amesema utaratibu huo umeanza kuondoa dhana kwamba TRA ni adui wa walipa kodi, badala yake umejenga mazingira ya ushirikiano na maelewano.
Amesema hali hiyo inawapa wawekezaji imani ya kuendelea kufanya biashara na kuwekeza nchini kutokana na kuona mazingira ya kodi yakizidi kuwa rafiki.
Naye Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya, amepongeza mfumo wa IDRAS kwa kurahisisha ulipaji kodi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kikodi.








