Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa imeendesha mafunzo kwa wajumbe wa Bodi za Usuluhishi wa Ndoa katika ngazi ya Kata kwa lengo la kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kusaidia kupunguza mashauri mahakamani pamoja na migogoro ya ndoa katika jamii.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa pamoja na Ukumbi wa Passion Hotel uliopo kata ya Nkwenda, yakihusisha Wajumbe wa Bodi za Usuluhishi kutoka kata zote za Wilaya ya Kyerwa.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, SACF. James John, amesema washiriki hao wana wajibu wa kulinda na kudumisha mshikamano katika kusuluhisha mashauri ya ndoa kwa lengo la kuhakikisha familia zinaishi kwa amani na kudumu.
“Taifa imara linategemea jamii imara, na jamii imara inategemea familia imara ambayo ni matokeo ya ndoa tulivu. Hivyo wajibu wenu siyo tu kutatua migogoro, bali pia kuhakikisha mnatoa ushauri utakaosaidia kupunguza migogoro ya kifamilia,” amesema SACF. John.
Aidha, ameeleza kuwa kuvunjika kwa familia husababisha athari mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo kupungua kwa kipato cha familia, kuongezeka kwa mzigo wa malezi, pamoja na kuathiri ustawi na malezi ya watoto na kutoa rai kwa wajumbe hao kuweka mikakati madhubuti katika kushughulikia suhulu za ndoa na kulinda haki za familia.



Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa, Musa Gumbo, ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mafunzo hayo, huku akiomba yawe endelevu ili kusaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika ndoa na familia.
Amesema anaamini mafunzo hayo yatachangia kujenga familia na ndoa imara, jambo litakalosaidia kujenga jamii yenye mshikamano na kuwawezesha wananchi kujikita zaidi katika shughuli za uzalishaji badala ya migogoro.
Naye Wakili Peter Mbogoro, Muwezeshaji kutoka Wizara ya Katiba na Sheria amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha bodi za usuluhishi zinatekeleza majukumu yao kikamilifu katika kutatua changamoto za wananchi, hususan katika eneo la usuluhishi wa migogoro ya kifamilia.
Ameongeza kuwa taasisi yoyote huanzia kwenye familia, hivyo wizara imeamua kuziimarisha bodi hizo ili ziwe sehemu muhimu ya ujenzi wa jamii imara na yenye amani.






