Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao na ujumbe wa Taasisi ya WaterAid UK ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Kusini mwa Afrika, Robert Kampala, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 61 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mkutano Mkuu wa 52 wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF), unaoendelea jijini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo.
Katika kikao hicho, Serikali ya Tanzania na WaterAid UK zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika maendeleo ya huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (WASH).




Ushirikiano huo unalenga kuimarisha mifumo ya kitaasisi, kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kuongeza uwekezaji unaohimili mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta hiyo muhimu.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dk. Natu El-maamry Mwamba, ambaye pia ni Gavana Mbadala wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Rished Bade, Kamishna Msaidizi wa Idara hiyo Robert Mtengule pamoja na maafisa wengine wa Wizara ya Fedha.
Kwa upande wa WaterAid UK, walihudhuria pia Mkurugenzi wa Pan Africa Advocacy, Dk. Tanko Yussif Azzika pamoja na maafisa wengine wa taasisi hiyo.





