Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imesema uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi, ukichochewa na maboresho ya sera, mageuzi mbalimbali na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa leo, Jumanne Juni 9, 2026 na Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, alipozungumza katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Singapore.
Kongamano hilo, limehudhuriwa na Rais Samia na Rais, Tharman Shanmugaratnam aliyepo nchini kwa ziara ya siku tatu.
Alisema Tanzania ina fursa nyingi kwa Singapore kuleta mtaji, teknolojia na utaalamu kwa kushirikiana na kampuni za ndani, hususan katika sekta za teknolojia, huduma za kifedha, usafirishaji, ugavi na nishati zinazoendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
“Kuna nafasi kubwa kwa Singapore kuleta mtaji, teknolojia na utaalamu ili kushirikiana na kampuni za Kitanzania,” amesema Angelina.
Ameeleza ingawa Serikali zina jukumu muhimu la kuweka mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji, ni wafanyabiashara na kampuni binafsi ndizo zinazopaswa kutumia fursa hizo kuzalisha bidhaa na kukuza kiuchumi.
“Serikali inaweza kufungua milango, lakini ni biashara na kampuni ndizo zinazopaswa kuingia na kutumia fursa hizo,” amesema.
Aidha, amesema majukwaa ya ushirikiano kati ya serikali kama vile tume za pamoja na mabaraza ya biashara yana mchango mkubwa katika kuweka mifumo, makubaliano, itifaki na kujenga mahusiano mema kati ya nchi, lakini biashara na uwekezaji wa kweli hutegemea hatua zinazochukuliwa na sekta binafsi.
“Majukwaa haya huweka mifumo, makubaliano, itifaki na kuimarisha mahusiano mema, lakini biashara na uwekezaji halisi utafanywa na kampuni za sekta binafsi,” amesema.




