Kampuni ya Airtel Africa plc, inayotoa huduma ya mawasiliano ya simu na huduma za kifedha kwa njia ya simu katika nchi 14 barani Afrika, imefanikiwa kuokoa lita milioni 9.1 za mafuta mazito ya dizeli katika mwaka wake wa kifedha wa 2025/2026 uliomalizika hivi karibuni.
Hatua hiyo ni sehemu ya mikakati madhubuti ya Airtel Afrika katika kuchochea ukuaji wa uchumi unaozingatia uwajibikaji, kwa kupunguza athari za mazingira zinazotokana na shughuli zake za kila siku.
Mafanikio hayo yamefikiwa kupitia mpango wa kupunguza utegemezi wa mafuta ya dizeli na kuongeza matumizi ya vyanzo vya nishati mbadala vyenye kiwango kidogo cha kaboni. Katika kipindi hicho, Airtel Africa ilifanikiwa kuhamishia vituo vya miundombinu (minara) 390 kwenye mfumo wa nishati ya umeme wa gridi ya taifa, hatua iliyoongeza ufanisi na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Akiwasilisha Ripoti ya Tathmini ya Uendelevu (Sustainability Scorecard) kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Lusaka, Zambia, Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa Airtel Africa, Sunil Taldar, aliangazia maendeleo yaliyofikiwa kuelekea kujenga Afrika endelevu, jumuishi na yenye mawasiliano ya uhakika.
Mbali na nishati, Airtel Africa ilitangaza kupiga hatua kwenye uhifadhi wa mazingira kupitia mfumo wa ‘uchumi rejereshi’ (circular economy), ambapo ilifanikiwa kurejeleza (recycling) asilimia 94 ya taka zote zilizozalishwa na kampuni. Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa Airtel Africa unaolenga kusawazisha ukuaji wa kibiashara, utunzaji wa mazingira, ujumuishi wa kidijitali, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Bw. Taldar alisisitiza kuwa ukuaji unaozingatia uendelevu wa mazingira ndio nguzo kuu ya mkakati wao wa biashara, jambo linaloiwezesha Airtel Afrika kupanua huduma na fursa kwa mamilioni ya Waafrika. Kwa sasa, mtandao wa Airtel Africa unafikia asilimia 81.9 ya idadi ya watu katika masoko yake, hatua inayorahisisha ufikiaji wa habari, elimu, na fursa za kiuchumi kwa jamii nzima.
Katika sekta ya kifedha, kampuni hiyo imerekodi maendeleo makubwa ambapo huduma ya Airtel Money sasa inahudumia wateja milioni 54.1 kupitia mtandao mpana wa mawakala milioni 2.4. Hali hii inaifanya Airtel Money kuwa moja ya mifumo mikubwa zaidi ya kidijitali ya kifedha barani Afrika.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa asilimia 44.1 ya wateja wote wa Airtel Money ni wanawake, takwimu inayothibitisha mchango mkubwa wa jukwaa hilo katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia huduma za kifedha zilizo salama, nafuu, na rahisi.
Kupitia taasisi yake ya kutoa misaada ya ‘Airtel Africa Foundation’, Airtel Afrika imewekeza dola za Kimarekani milioni 6.2 (zaidi ya shilingi bilioni 17) katika programu za kipaumbele kwenye maeneo manne ya kimkakati: Ujumuishi wa Kifedha, Elimu, Uendelevu wa Mazingira, na Ujumuishi wa Kidijitali.
Kupitia ushirikiano wake na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), jumla ya shule 3,296 zimeunganishwa na mtandao wa intaneti wa bure, hatua inayosaidia kuziba pengo la kidijitali na kutoa elimu bora kwa wanafunzi zaidi ya milioni 2 na walimu 38,868. Aidha, majukwaa 64 ya kujifunzia ya kidijitali yasiyotoza gharama za data (zero-rated) yaliwawezesha zaidi ya wanafunzi milioni 11 kupata maudhui ya elimu bure.
Katika kukuza vipaji, zaidi ya vijana 30,000 walipata mafunzo ya ujuzi wa kidijitali, huku ufadhili kamili wa masomo ya shahada ya kwanza (undergraduate STEM scholarships) zaidi ya 250 ukitolewa kupitia programu ya Airtel Africa Tech Fellowship, lengo likiwa ni kuandaa kizazi kijacho cha wavumbuzi na viongozi wa teknolojia barani Afrika.
Ripoti kamili ya Uendelevu ya Airtel Africa ya mwaka 2026 inapatikana katika tovuti yao ya www.airtel.africa.




