HomeHabariMagambo: Kaulimbiu ya PSSSF ‘Tunalipa Jana’ yaleta furaha kwa wastaafu

Magambo: Kaulimbiu ya PSSSF ‘Tunalipa Jana’ yaleta furaha kwa wastaafu

Dar es Salaam, Julai 4, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Fortunatus Magambo, amesema kaulimbiu ya “Tunalipa Jana” iliyoanzishwa na Mfuko huo mwezi Aprili mwaka huu imeendelea kuleta faraja kwa wanachama wanaostaafu, ambapo wengi wao wenye nyaraka zilizokamilika na kuwasilishwa kwa wakati wamelipwa mafao yao kabla mara tu baada ya kustaafu.

‎Magambo amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alijionea namna Mfuko unavyotoa huduma kwa wananchi na wanachama kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA. Aidha, alitembelea mabanda ya Benki ya Azania na Watumishi House.

‎Amesema kaulimbiu ya “Tunalipa Jana” inaakisi dhamira ya PSSSF ya kuboresha huduma kwa wanachama kwa kuhakikisha kila anayekidhi vigezo analipwa mafao yake kwa wakati.

‎”Tunapoanza kumsajili mwanachama, tunahakikisha taarifa zake zinakuwa sahihi na zinahuishwa kila inapobidi. Lengo letu ni kwamba anapofikia umri wa kustaafu asiwe na changamoto yoyote ya malipo. Tunataka alipwe siku ya kustaafu. Hiyo ndiyo tafsiri halisi ya kaulimbiu yetu ya Tunalipa Jana,” amesema Magambo.



‎Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2026/2027 ulioanza mwezi Julai, PSSSF tayari imeanza kuchakata nyaraka za watumishi wanaokaribia kustaafu ili kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati mara wanapomaliza utumishi wao.

‎Kwa mujibu wa Magambo, mafanikio hayo yamewezeshwa pia na kuimarika kwa ukwasi wa Mfuko kufuatia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kulipa deni la muda mrefu la michango ya wanachama lililokuwa likiidai Serikali.

‎”Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ulipaji wa deni hilo. Serikali imelipa zaidi ya shilingi trilioni nne, jambo ambalo limeongeza ukwasi wa Mfuko na kutuwezesha kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, ikiwemo kulipa mafao ya wanachama kwa wakati,” amesema.

‎Amesisitiza kuwa PSSSF itaendelea kuwekeza katika mifumo ya TEHAMA, kuboresha huduma kwa wanachama na kuimarisha ushirikiano na waajiri ili kuhakikisha kaulimbiu ya “Tunalipa Jana” inatekelezwa kikamilifu na kila mwanachama anayestahili anapata mafao yake kwa haraka, kwa wakati na kwa ufanisi.



‎Akitoa ushuhuda wake kuhusu utekelezaji wa kaulimbiu hiyo, mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rosemary Makene, amesema alipata mafao yake ya mkupuo mara tu baada ya tarehe yake ya kustaafu kufika, jambo ambalo hakulitegemea kutokana na uzoefu aliokuwa akiusikia hapo awali.

‎”Sikupata usumbufu wowote. Niliwasilisha madai yangu kwa njia ya mtandao na nilikuwa nafuatilia hatua zote za uchakataji wake hadi nilipopokea malipo yangu. Kwa kweli PSSSF wanafanya kazi nzuri sana. Sisi wastaafu tunawashukuru. Baada ya kustaafu, mwajiri anakamilisha jukumu lake, lakini PSSSF ndiyo inabaki kuwa mshirika wako katika maisha ya ustaafu. Nawapongeza kwa huduma bora wanayoendelea kuitoa,” amesema Rosemary.

‎Kaulimbiu ya “Tunalipa Jana” ni sehemu ya mkakati wa PSSSF wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama kupitia matumizi ya teknolojia, kuimarisha mifumo ya utunzaji wa taarifa za wanachama na kuongeza ufanisi katika uchakataji wa mafao, ili kuhakikisha wanachama wanapata stahiki zao kwa wakati.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments