HomeHabariKampeni ya Tunalipa Jana;  Tayari PSSSF imewatambua watumishi 7,881 watakaostaafu 2026/27

Kampeni ya Tunalipa Jana;  Tayari PSSSF imewatambua watumishi 7,881 watakaostaafu 2026/27


Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishji wa Umma (PSSSF), Hajj Khamisi amesema katika kuhakikisha azma ya kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’ inatekelezwa kwa ufanisi, tayari Mfuko umewatambua Wanachama 7,881 wanaotarajiwa kustaafu utumishi wa Umma katika mwaka huu wa fedha 2026/27. 

Amesema hayo katika Banda la PSSSF kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.

“ Tulikwishawasiliana na waajiri tangu mwezi Machi, 2026 kwa kuwapatia orodha (majina) na tarehe za kustaafu kwa watumishi hao,“ amesema huku akiwashukuru waajiri kwa kuonyesha ushirikiano  kwa kuwasilisha madai ya watumishi kwa wakati hatua inayourahisishaia  Mfuko kuyachakata madai hayo kwa wakati.

“Hii itasaidia azma ya Mfuko kutekeleza kaulimbiu yake ya ‘Tunalipa jana’ na hivyo kuwaletea tabasamu wastaafu wetu,” amesema.

Akizungumzia mkakati wa kuhakikisha Mfuko unatekeleza kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’, Mkurugenzi wa TEHAMA, Eric Kato, amesema mifumo ya TEHAMA ya Mfuko imeimarishwa kwa kiasi kikubwa hali inayosaidia uharakishwaji wa utoaji huduma.

“ Kupitia Mifumo, mwanachama anaweza kuwasilisha madai yake mahali popote alipo, hawahitaji kusafiri na hivyo wanaokoa fedha lakini pia Serikali kupitia Mfuko imeokoa fedha nyingi hususan za manunuzi ya karatasi, kwani karibu asilimia 100 ya huduma zinatolewa kupitia mtandao.” amesisitiza.

Aidha Mkurugenzi wa Fedha, PSSSF, Ally Yakiti, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dk Samia Suluhu Hassan, imeuwezesha Mfuko kwa kuwasilisha michango bila kuchelewesha.

“ Hakuna sababu yoyote kwa Mwanachama pindi anapostaafu acheleweshewe Mafao yake yawe ya Mkupuo au Pensheni ya kila mwezi, tuna slogan ya tunalipa jana tukimaanisha kwamba Mwanachama hacheleweshwi kupata haki zake pindi anapotimiza wajibu wake,” amefafanua.

Kwa upande wao, wastaafu wanaopokea pensheni kupitia Mfuko huo, wamesema pensheni zao za kila mwezi wamekuwa wakipata kwa wakati.

“ Pensheni yangu napata vizuri, tarehe 22 wakati mwingine tarehe 23 au 24 haijawahi kuchelewa, nashukuru sana,” amesema Margareth Onjari 

“ Tena wakati mwingine pensheni inawahi mfano mwezi uliopita imewahi vizuri sana, nafikiri labda ni kwa sababu ya maendeleo ya kiteknolojia, sijaona tatizo lolote PSSSF.” amesema Mstaafu mwingine Said Mohammed.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments