Wafugaji nchini wanatarajiwa kunufaika na mfumo wa kisasa wa biashara ya mifugo baada ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kuanza kuingiza mifugo katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, hatua itakayowezesha biashara kufanyika kwa uwazi na ushindani kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu, amesema hatua hiyo ni sehemu ya upanuzi wa huduma za bodi baada ya mafanikio yaliyopatikana katika kusimamia biashara ya mazao ya kilimo kupitia mfumo huo.
Amesema hadi sasa WRRB inasimamia bidhaa 18 za mazao ya kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, na sasa imeanza kujumuisha sekta ya mifugo ili wafugaji nao wanufaike na mfumo huo.
Kwa mujibu wa Bangu, mifugo itasajiliwa kidijitali na kuingizwa kwenye mfumo, hatua itakayowezesha wanunuzi kushindana kwa uwazi kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), kuongeza uwazi wa bei na kupanua masoko kwa wafugaji.
Amesema uamuzi wa kuingiza mifugo umetokana na maombi ya wadau wa sekta hiyo ambao walitaka kuona mfumo wa Stakabadhi za Ghala unawanufaisha pia wafugaji, badala ya kuendelea kuhudumia wakulima pekee.
“Baada ya mafanikio tuliyoyapata katika mazao ya kilimo, sasa tumepanua mfumo huu kwa sekta ya mifugo ili wafugaji nao wanufaike na fursa za biashara ya kisasa, yenye uwazi na ushindani wa soko,” amesema Bangu.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inatarajiwa kuongeza thamani ya mifugo, kuboresha upatikanaji wa masoko na kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao kwa bei shindani kupitia mfumo wa kidijitali.




