Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ikiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Mhe. Dkt. Emanuel Qambaji Nuwas, na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Yeconia Deles, tarehe 06 Julai 2026 wametembelea banda la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Wakiwa katika banda la TVLA lililopo ndani ya banda la pamoja la Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliweza kupata elimu kuhusiana na huduma mbalimbali zinazotolewa na TVLA kuhusiana na jinsi ya kuimarisha afya ya mifugo, kupitia udhibiti wa magonjwa ya mifugo pamoja uhakiki wa ubora wa chakula cha mifugo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Dkt. Nuwas alisema ameridhishwa na kiwango cha huduma zinazotolewa na TVLA, hususan huduma za uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, uzalishaji wa chanjo pamoja na matumizi ya teknolojia za maabara katika kudhibiti na kuzuia magonjwa ya mifugo.


Alisema huduma zinazotolewa na TVLA zina mchango mkubwa katika kuongeza tija ya ufugaji na kuinua uchumi wa wafugaji, huku akiitaka TVLA kuendelea kuongeza juhudi za kuwafikia wafugaji wengi zaidi nchini kuwapatia elimu na mafunzo kuhusu umuhimu wa huduma za maabara.
“TVLA inaendelea kufanya kazi kubwa ya kulinda afya ya mifugo yetu. Nawapongeza kwa huduma hizi muhimu na nitoe rai muendelee kuwafikia wafugaji wengi zaidi muwapatie elimu na huduma za kitaalamu ili sekta ya mifugo ichangie zaidi katika uchumi wa wananchi na Taifa,” alisema Mhe. Dkt. Nuwas.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Mhe. Yeconia Deless Maleyecky, aliwataka madiwani walioambatana naye kutumia elimu waliyoipata katika banda la TVLA kuwahamasisha wananchi katika kata zao kuhusu umuhimu wa kinga na udhibiti wa magonjwa ya mifugo.
Alisema viongozi wa serikali za mitaa wana nafasi kubwa ya kuwaelimisha wafugaji kuhusu matumizi ya chanjo, uchunguzi wa magonjwa na huduma nyingine zinazotolewa na TVLA, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mifugo na kuboresha vipato vya wananchi.
Akitoa maelezo kwa viongozi hao, Daktari Mtafiti wa Mifugo kutoka TVLA, Dkt. Julius Mwanandota, alisema TVLA ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi yenye jukumu la kulinda afya ya mifugo kupitia huduma za kisasa za maabara, utafiti na uzalishaji wa chanjo.
Dkt. Mwanandota alieleza kuwa TVLA hutoa huduma za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo kwa kutumia teknolojia za kisasa za maabara, huzalisha na kusambaza chanjo za mifugo, pamoja na kufanya uchunguzi wa ubora na usalama wa vyakula vitokanavyo na mifugo.
Aidha, alisema Wakala hufanya usajili na uhakiki wa ubora wa viuatilifu vya mifugo kabla ya kuruhusiwa kutumika nchini, kufanya tafiti kuhusu magonjwa ya mifugo, na kutoa huduma za ushauri na mafunzo kwa wanafunzi, wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo.
Katika Maonesho hayo, banda la TVLA limeendelea kuwa kivutio kwa wageni mbalimbali wanaotembelea Sabasaba, ambapo hupata elimu kuhusu huduma za uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, uzalishaji wa chanjo, usalama wa bidhaa zitokanazo na mifugo na huduma nyingine za kitaalamu zinazolenga kuongeza tija ya ufugaji na kuchangia maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.






