ZANZIBAR – Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuvuna matunda ya uwekezaji katika sekta ya elimu baada ya matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita wa mwaka 2026 kuonyesha ufaulu wa asilimia 99.37, huku wanafunzi wengi wakipata sifa za kujiunga na vyuo vikuu.
Akizungumza leo katika Ofisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mazizini, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, amesema watahiniwa 5,161 waliandikishwa kufanya mtihani kutoka shule 57 za serikali na binafsi, ambapo wanafunzi 5,130 walifanya mtihani, sawa na asilimia 99.34 ya walioandikishwa.
Amesema kati ya waliofanya mtihani huo, wanafunzi 5,098 walifaulu, sawa na asilimia 99.37, kiwango kinachoonyesha kuendelea kuimarika kwa ubora wa elimu nchini Zanzibar.
“Mafanikio haya ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuimarisha uwezo wa walimu pamoja na kuongeza miundombinu ya elimu,” amesema Waziri Lela.
Amesema wanafunzi 4,979, sawa na asilimia 97.21 ya waliofaulu, wamepata madaraja ya Kwanza hadi Tatu, hivyo kufuzu kujiunga na vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi, huku wanafunzi 119 waliopata Daraja la Nne wakistahili kuendelea na masomo ya ngazi ya stashahada.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mwaka huu umeweka rekodi mpya ya idadi ya wanafunzi waliopata Daraja la Kwanza, ambapo wameongezeka kutoka 922 mwaka 2025 hadi 1,304 mwaka 2026, sawa na ongezeko la asilimia 41.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa wanafunzi wa kike wameendelea kufanya vizuri zaidi, wakirekodi ufaulu wa asilimia 99.7 ikilinganishwa na asilimia 99.5 kwa wanafunzi wa kiume.
Katika masomo mbalimbali, Sayansi ya Kompyuta, Biashara, Lishe na Ustawi wa Familia, Elimu ya Michezo, Lugha ya Kifaransa na Sanaa ya Uchoraji yalirekodi ufaulu wa asilimia 100.
Hata hivyo, Waziri Lela amesema bado kuna changamoto katika masomo ya Basic Applied Mathematics (BAM) na General Studies (GS), ambayo yalipata ufaulu wa asilimia 36.25 na asilimia 44.48 mtawalia.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuboresha ufundishaji wa masomo hayo ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika miaka ijayo.




