HomeBiasharaTRA, NBAA waendesha mafunzo mabadiliko ya Sheria za Kodi 2026/27 kuleta uelewa...

TRA, NBAA waendesha mafunzo mabadiliko ya Sheria za Kodi 2026/27 kuleta uelewa kwa walipa kodi 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), imeanza mafunzo maalumu kwa wahasibu, wakaguzi, washauri wa kodi na wataalamu wa fedha kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi yaliyomo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2026/27.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi, CPA Paul Walalaze, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uelewa wa mabadiliko hayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa usahihi na kuwashauri walipakodi ipasavyo.

CPA Walalaze amesema mabadiliko hayo yanahusu sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sheria ya Usajili wa Vyombo vya Moto, Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sheria ya Ushuru wa Stempu na Sheria ya Uingizaji wa Bidhaa Nchini.

Ameeleza kuwa semina hizo pia zinatoa nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika utekelezaji wa sheria za kodi.



Aidha, amesema TRA itaendelea kutumia elimu ya kodi kama nyenzo ya kuongeza wigo wa walipakodi na kuimarisha utamaduni wa ulipaji wa kodi kwa hiari. 

Amebainisha kuwa ulipaji wa kodi kwa hiari unategemea kujisajili na kupata TIN, kuwasilisha makadirio na ritani kwa wakati, kulipa kodi kwa wakati, kutunza kumbukumbu sahihi za biashara, kutumia mifumo ya kielektroniki kwa usahihi na kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na walipakodi.
 
Pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya usimamizi wa kodi nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, Prof. Siasa Mzenzi, amesema ushirikiano kati ya NBAA na TRA umeendelea kuimarisha elimu ya kodi kwa wahasibu na wafanyabiashara. 

Ameeleza kuwa semina hizo zinaongeza uelewa wa wataalamu wa fedha kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi, kuwawezesha kuwashauri walipakodi kwa usahihi na kuchangia kuongezeka kwa ulipaji wa kodi kwa hiari, jambo linaloongeza mapato ya Serikali na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments