HomeBiasharaWRRB yapokea tuzo ya mchango katika utafiti wa kilimo

WRRB yapokea tuzo ya mchango katika utafiti wa kilimo

DODOMA – Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetunukiwa tuzo maalumu kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha utafiti kuhusu maboresho ya kisasa ya mnyororo wa thamani wa kilimo uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo ya Canada (IDRC-CRDI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Tuzo hiyo imekabidhiwa leo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu, pamoja na Meneja wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Elfaraja Kintingu, ikiwa ni kutambua mchango wa Bodi katika kuendeleza maboresho ya mfumo wa biashara ya mazao nchini.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bangu alisema heshima hiyo ni uthibitisho wa nafasi muhimu ambayo WRRB imeendelea kuwa nayo katika kuimarisha sekta ya kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Alisema mfumo huo umechangia kuongeza ufanisi wa biashara ya mazao, kuimarisha uwazi wa masoko, kuongeza ushindani wa bei na kuboresha upatikanaji wa masoko kwa wakulima ndani na nje ya nchi.

“Hii ni heshima kwa WRRB na wadau wote tunaoshirikiana nao. Itaendelea kutupa nguvu ya kuimarisha ubunifu na mifumo inayochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na kuongeza tija kwa wakulima,” alisema Bangu.

Aliongeza kuwa WRRB itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti, vyuo vikuu na wadau mbalimbali ili kuendeleza tafiti na ubunifu unaoboresha mnyororo wa thamani wa kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Awali, Meneja wa TEHAMA wa WRRB, Elfaraja Kintingu, alisema tuzo hiyo imetolewa kutokana na ushirikiano na mchango wa Bodi katika kufanikisha utafiti huo, ambapo watafiti walitembelea maghala mbalimbali nchini kujionea utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na mchango wake katika kuimarisha biashara ya mazao, kuongeza uwazi wa masoko na kuboresha mnyororo wa thamani wa kilimo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments