HomeHabariSamia apongezwa kwa kuipa kipaumbele sekta ya maji

Samia apongezwa kwa kuipa kipaumbele sekta ya maji

Tanzania imeeleza hatua zinazochukuliwa kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama, ikiwamo uwekezaji katika miradi ya maji na kuimarisha usimamizi wake, katika mkutano wa viongozi wa Afrika unaofanyika Luanda, Angola.

Mkutano huo, unaowakutanisha marais, mawaziri wa mambo ya nje na mawaziri wa maji, unajadili nafasi ya rasilimali za maji katika kujenga amani na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za Afrika.

Viongozi walioshiriki mkutano huo wameeleza umuhimu wa uongozi na uwekezaji katika sekta ya maji, wakati Tanzania ikiwasilisha hatua zinazochukuliwa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha huduma hiyo na kupeleka miradi katika maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa maji.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa Oktoba 22, 2026, unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Mahmoud Thabit Kombo, anayemwakilisha Rais Samia. Ujumbe huo pia unajumuisha Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, pamoja na wataalamu wengine.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni *“Kuimarisha Utawala wa Rasilimali Maji Inayovuka Mipaka Barani Afrika kama Nyenzo ya Kuzuia na Kutatua Migogoro.”

Majadiliano yamejikita katika diplomasia ya maji na usimamizi wa rasilimali zinazovuka mipaka, ushiriki wa jamii, wanawake na vijana, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, uhamaji wa watu na migogoro.

Washiriki pia wanajadili uwekezaji katika miundombinu ya maji na kujenga uwezo wa taasisi na wadau wanaohusika na usimamizi wa rasilimali hizo.

Kupitia jukwaa hilo, Tanzania inawasilisha uzoefu na hatua zilizopigwa katika sekta ya maji, huku ikieleza mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na usimamizi wa pamoja wa mabonde ya mito na maziwa.

Mkutano huo unatoa fursa kwa nchi za Afrika kujadili namna ya kutumia rasilimali za maji kwa ushirikiano, kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments