HomeHabariMasauni akagua maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko Kigoma

Masauni akagua maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko Kigoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yusuf Masauni, amekagua maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuahidi kuwa Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili wananchi ili kupunguza athari za mafuriko.

Katika ziara yake iliyofanyika Oktoba 17, 2026, Masauni ametembelea maeneo ya Kibirizi na Katubuka, ambako amejionea athari za mafuriko na uharibifu wa mazingira.

Akiwa Katubuka, amewapa pole wananchi walioathirika na kuwaeleza kuwa Serikali itaendelea kutafuta suluhisho la changamoto hiyo kwa kuzingatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Masauni amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mafuriko, ikiwamo kuhamia maeneo salama pale inapohitajika, pamoja na kushirikiana na viongozi wa maeneo yao katika kutekeleza hatua za kukabiliana na athari hizo.

Aidha, amekagua ujenzi wa mtaro unaolenga kuelekeza maji kutoka Katubuka kwenda Ziwa Tanganyika, hatua inayotarajiwa kusaidia kupunguza mkusanyiko wa maji na athari zake katika makazi ya wananchi.

Akisisitiza dhamira ya Serikali katika kutatua changamoto hiyo, Masauni amesema Serikali imejipanga kuchukua hatua za vitendo ili kulinda maisha na mali za wananchi.

“Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan si Serikali ya mchakato na maneno, bali ni Serikali ya vitendo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk. Rashid Chuachua, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema Manispaa ya Kigoma Ujiji ilipata mvua zilizozidi wastani katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025, hali iliyosababisha athari mbalimbali.

Amesema maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa ni Kata za Katubuka, Kibirizi, Bangwe na Buzebazeba, ambako maji yaliingia katika nyumba zilizokuwa karibu na Bwawa la Katubuka.

Chuachua amesema Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mafuriko na umuhimu wa kuepuka maeneo hatarishi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments