HomeBiasharaPPAA: Malalamiko ya zabuni sasa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao

PPAA: Malalamiko ya zabuni sasa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeimarisha upatikanaji wa haki kwa wazabuni kupitia mifumo ya kidijitali inayorahisisha uwasilishaji wa malalamiko na rufaa, hatua inayolenga kupunguza gharama, kuokoa muda na kuongeza uwazi katika michakato ya ununuzi wa umma.

Hatua hiyo imeelezwa na Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Sheria wa PPAA, Agnes Sayi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Sita wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), unaofanyika Arusha kuanzia Oktoba 20 hadi 23, 2026.

Sayi, aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo katika mkutano huo unalenga kutoa elimu kwa wabunifu wa majengo, wakadiriaji majenzi na wadau wengine kuhusu haki zao wanaposhiriki michakato ya zabuni za umma.

Amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 iliweka sharti la ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya kielektroniki kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), hatua iliyochochea PPAA kuanzisha moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa.

“Baada ya kuanza rasmi kwa matumizi ya moduli hiyo, uwasilishaji wa malalamiko umerahisishwa na kutoa fursa kwa wazabuni wengi zaidi, huku ikiokoa muda na gharama, kuongeza uwazi na uwajibikaji, na kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu za malalamiko na rufaa,” amesema Sayi.

Ameeleza kuwa kabla ya mfumo huo kuanza kutumika, wazabuni wasiokubaliana na maamuzi ya maafisa masuuli au taasisi nunuzi walilazimika kuwasilisha malalamiko au rufaa moja kwa moja katika ofisi za PPAA jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Sayi, utaratibu huo ulikuwa ukihitaji muda na gharama zaidi, huku ukisababisha changamoto za upotevu wa baadhi ya nyaraka na kuathiri ufanisi wa utunzaji wa kumbukumbu.

Amesisitiza kuwa mazingira ya haki katika zabuni za umma yanahitaji washiriki wote kutendewa kwa usawa bila upendeleo, kwa kuzingatia sheria, kanuni na masharti yaliyowekwa katika nyaraka za zabuni. Pia, amesema mchakato huo unapaswa kuzingatia uwazi na uadilifu na kupinga vitendo vya rushwa.

Katika hatua nyingine, Sayi amesema PPAA imeanzisha huduma ya kusikiliza mashauri kwa njia ya mkutano wa video (video conference) ili kuwawezesha wahusika wanaoshindwa kufika katika ofisi za mamlaka hiyo kushiriki katika usikilizaji wa mashauri yao.

Amesema huduma hiyo imewezesha baadhi ya mashauri kusikilizwa huku washiriki wakiwa katika mikoa mbalimbali nchini na katika mataifa mengine, yakiwamo Afrika Kusini, Nigeria, Poland, India na China.

Aidha, PPAA imeanzisha programu ya simu za mkononi (mobile app) inayowawezesha wazabuni kuwasilisha malalamiko na rufaa dhidi ya maamuzi yanayotolewa katika michakato ya ununuzi wa umma. Hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza gharama zinazohusiana na kudai haki.

Sayi amewahimiza wabunifu wa majengo, wakadiriaji majenzi na wadau wengine kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi wa umma ili kuimarisha ushindani, matumizi bora ya fedha za umma na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Mkutano Mkuu wa Sita wa AQRB unaongozwa na kaulimbiu: “Kuijenga Tanzania Tunayoitaka Kuelekea 2050: Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kwa Mazingira Endelevu ya Ujenzi.”

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments