Watanzania na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasishwa kushirikiana na Serikali ili kufanikisha malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Wito huo umetolewa leo Agosti 20, 2025 jijini Mbeya na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Florian Haule, wakati wa hafla ya kugawa mitungi ya gesi ya kilo 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mbeya, zoezi linalotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Haule, akiwa ameambatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Stephen Mwakifwamba, aliwataka maafisa na askari wa Jeshi la Magereza kushirikiana na Serikali kwa kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Tunapenda kuendelea kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo inalenga kuboresha maisha ya wananchi na kutunza mazingira. Serikali pekee haiwezi kufanikisha mkakati huu, hivyo tuendelee kuwahamasisha ndugu, jamaa na jamii inayotuzunguka ili tufanikishe lengo la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema Haule.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya, alisema kuwa REA imeingia makubaliano na Jeshi la Magereza kutekeleza mradi wa kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza yote nchini.




Ameeleza kuwa mradi huo unaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 35, ambapo kati yake zaidi ya Shilingi Bilioni 26.5 zimetolewa na REA kwa ajili ya kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza yote pamoja na kugawa mitungi ya gesi na majiko ya kisasa kwa watumishi wa jeshi hilo.
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Francis Manyama kutoka REA alisema kuwa katika Mkoa wa Mbeya pekee, jumla ya mitungi 895 ya gesi ya kilo 15 na majiko ya sahani mbili inatarajiwa kugaiwa kwa watumishi wa Jeshi la Magereza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Raymond Mwampashi, aliishukuru Serikali kwa msaada huo na kuahidi kuwa watumishi wote wa jeshi hilo wataendelea kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.











