Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupata uchunguzi, ushauri na matibabu ya kibingwa kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Mama Samia, waliopiga kambi ya siku tano mkoani humo.
Mhita ametoa wito huo leo Oktoba 13, 2025, wakati wa kuwapokea Madaktari Bingwa 36 waliowasili mkoani humo, ambao wamesambazwa katika halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga.
Amesema madaktari hao wamekuja kwa lengo la kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi, hivyo ni fursa kwa wakazi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma hizo.



“Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wajitokeze kwa wingi kwenye kambi hii ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia, ambao wameweka kambi kwa muda wa siku tano mfululizo ili kufanya uchunguzi, kutoa ushauri na matibabu ya kibingwa,” amesema Mhita.
Aidha, Mhita amesema hii ni awamu ya nne ya kambi ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia kufanyika mkoani humo, na kwamba hadi sasa wamehudumia wananchi zaidi ya 240,000 na kujengea uwezo wataalamu 15,000 wa halmashauri.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kambi hiyo Michael Mbele, amesema wamejipanga vizuri kutoa huduma bora kwa wananchi wa Shinyanga, na wanatarajia kuwafikia zaidi ya watu 30,000 katika kipindi hicho cha siku tano.




