Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, amesema ushiriki wa wananchi na wadau mbalimbali katika kuchangia huduma za afya ni muhimu ili kuimarisha matibabu ya upandikizaji uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Sickle Cell Disease pamoja na upandikizaji figo nchini.
Sillo amesema licha ya Tanzania kuanza kutoa huduma za upandikizaji figo na uloto ndani ya nchi, jambo lililosaidia kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi, bado huduma hizo zinahitaji uwekezaji mkubwa kutokana na gharama za matibabu na vifaa tiba.
Akizungumza katika hafla iliyowakutanisha viongozi wa Mkoa wa Dodoma, wabunge na wadau mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha mfuko wa kusaidia matibabu hayo, amesema magonjwa ya sickle cell na figo yanaweza kumkumba mtu yeyote bila kujali nafasi au hali ya maisha.


“Tunaposhiriki katika michango hii si kwa ajili ya taasisi moja, bali tunaunga mkono huduma za kitaifa zinazogusa maisha ya wananchi wengi wanaohitaji matibabu hayo,” amesema Sillo.
Amesema michango hiyo itasaidia kuboresha miundombinu ya afya, kuongeza uwezo wa utoaji huduma na kuwawezesha wagonjwa kupata matibabu kwa wakati.
Aidha, amesisitiza kuwa sekta binafsi, taasisi na wananchi wanapaswa kushirikiana na serikali katika kuimarisha huduma za kibingwa ili wagonjwa wanaohitaji upandikizaji viungo na matibabu maalumu waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi ndani ya Tanzania.






